WAKULIMA WASHAURIWA KUJIFUNZA TARI

  


Na Mwandishi Wetu


WAKULIMA wa mbogamboga, matunda, viungo na vikolezi wameshauriwa kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Tengeru ili kujifunza teknolojia bora za kilimo chenye tija.

Mwito huo umetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Kaimu Meneja wa TARI Tengeru, Dk. Happiness Mollel, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. Alisema taasisi hiyo imejikita katika utafiti wa mbegu bora za mazao hayo, hivyo wakulima wakitumia elimu inayotolewa wataongeza uzalishaji na kipato.

"TARI Tengeru tunazalisha mbegu bora za mbogamboga kama mchicha, ngogwe, nyanya na figiri. Pia tunahimiza ongezeko la thamani kwa mazao kupitia utengenezaji wa unga lishe kwa kutumia mahindi ya njano, mchicha nafaka na uwele. Uji wa mchanganyiko huu una protini nyingi na ni wenye lishe bora," alisema Dk. Mollel.

Aidha, alisema wamefanikiwa kuongeza thamani kwenye tunda la mizizi ya beet kwa kulitengenezea sharubati na hata kutengeneza mvinyo. Kwa upande wa viungo, alieleza kuwa nyanya ni zao lenye soko la uhakika, na kwamba wamefanikiwa kuimarisha uzalishaji wake kwa kutumia mbegu bora.

Alibainisha kuwa TARI imefanya utafiti wa mbegu za mchicha zinazokomaa kwa muda mfupi, hivyo kumuwezesha mkulima kupata kipato haraka. Alisisitiza umuhimu wa wakulima kujua afya ya udongo kabla ya kuanza kilimo, pamoja na kutumia mbegu bora kutoka taasisi zilizoidhinishwa kama ASA na TARI.

Kwa mujibu wa Dk. Mollel, TARI Tengeru ina mbegu mbalimbali za mchicha ikiwemo mchicha pori, akeri (mchicha nafaka), na nguruma (mchicha bwasi) ambao huvunwa kwa muda mrefu. Pia huzalisha mbegu za nyanya aina ya Tenguru 97, Tanya, Cheri na nyingine, ambazo zimeidhinishwa na TOSCI kwa ubora wake.

Aliongeza kuwa kwa kutumia mashamba darasa, kituo hicho kimeweza kuzalisha tani mbili za mbegu bora za mbogamboga.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa TARI Tengeru, Emmanuel Lasway, alisema mafanikio ya mkulima wa mbogamboga yanategemea kufuata kanuni sahihi za kilimo bora. Alisisitiza matumizi ya udongo usiotuamisha maji, kutengeneza vitalu vya miche kwa kutumia udongo wa msituni, na kuhakikisha maandalizi ya shamba yanakamilika kabla ya kupandikiza miche.

Lasway alieleza kuwa miche inapaswa kumwagiliwa hadi ifikie urefu wa sentimeta 5 hadi 10 kabla ya kupelekwa shambani. Aidha, alieleza kuwa katika upandaji wa bamia, matuta yanapaswa kuwa na umbali wa sentimeta 60 kati ya mistari na sentimeta 45 kati ya mche na mche. Kwa mazao mengine kama mchicha, mnavu na pilipili, umbali kati ya miche ni sentimeta 30.

Alishauri matumizi ya mbolea ya kuoteshea, ambapo gramu tano huwekwa kila shina baada ya kuchanganywa na udongo. Baada ya wiki mbili, mkulima anapaswa kuongeza gramu tano hadi 10 ya mbolea yenye kiwango kikubwa cha nitrojeni ili kupata mavuno bora.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya kilimo cha mbogamboga yanategemea upatikanaji wa maji ya kutosha, kudhibiti visumbufu na magugu shambani.


#kilimobora

#taritengeru

#wakulima

#mbegubora

#kilimokibiashara

#mchicha

#nyanya

#kilimolishe

#maendeleoyakilimo

#elimiyakilimo


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.