Wizara ya Kilimo imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa kilimo ikolojia pamoja na wakulima ili kuzalisha mbegu bora, salama na zinazokubalika sokoni. Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea, Twalib Njohole, wakati akifungua warsha ya siku tatu kuhusu nafasi ya mbegu za wakulima katika miongozo ya kisera.
Warsha hiyo imewakutanisha wadau wa mbegu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Senegal, Malawi, Uswisi, Zambia, Zimbabwe, Ethiopia na Umoja wa Ulaya (EU), ikiwa ni jukwaa la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Njohole alisema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa mbegu za wakulima na itaendelea kutoa ushirikiano kwa makundi yanayozalisha mbegu hizo kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbegu bora. Alibainisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo TARI, TOSCI na ASA, imekuwa ikiwezesha wakulima na wataalamu wa kilimo katika kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa wakati.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Baionuwai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi, alisema warsha hiyo inalenga kujadili nafasi ya mbegu za wakulima katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi na changamoto za uzalishaji wa chakula. Alieleza kuwa benki zaidi ya 30 za mbegu zimeanzishwa nchini, ishara ya matumaini kuwa jamii inaanza kuelekea kwenye matumizi ya mbegu za asili.
Mwakilishi Mkazi wa SWISSAID Tanzania, Betty Malaki, alisisitiza kuwa mbegu za wakulima ni salama kwa mazingira na watumiaji, huku akitoa wito kwa Serikali kuendelea kuzitambua na kuzilinda. Naye Mkurugenzi Mkazi wa Islands of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa, aliishukuru Serikali kwa kuthibitisha aina 17 za mbegu za wakulima, hatua inayowapa moyo kuendeleza jitihada hizo.
Dk. Atugonza Bilaro kutoka TARI alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kutambua mbegu za wakulima katika sera na sheria za nchi, akisema ni hatua muhimu katika kuhakikisha ustawi wa kilimo nchini.
---
#mbeguzaasili #kilimoendelevu #wakulima #wizayakilimo #tari #tosci #asa #swissaid #tabio #mbeguzawakulima #mabadilikoayatabianchi
Hakuna maoni: