WMA YAENDELEA KUUNGURUMA SABASABA: YATOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU VIPIMO, YASISITIZA “ULIZA, HAKIKI, THIBITISHA”

 


DAR ES SALAAM.

Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) umetoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajiridhisha na vipimo vinavyotumiwa na wafanyabiashara wanapowahudumia, ikiwa ni sehemu ya haki yao ya msingi kama walaji.


Akizungumza Julai 11, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA, Bi. Veronica Simba, alisema wananchi wana haki ya kuuliza na kuona uthibitisho wa vipimo vinavyotumika, ili kuondoa wasiwasi kuhusu usahihi wake.

 "Haki ya kuhoji ni ya kila mwananchi. Kama umeenda kwenye bucha na una mashaka na mzani uliotumika, usisite kuuliza na kujiridhisha kwamba mzani huo umehakikiwa na una stika ya Wakala wa Vipimo," alisema Bi. Simba.

Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wanajua kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi, lakini wanakosa ujasiri wa kuuliza au kuhoji, jambo linaloweza kuwapa hasara bila kujua.

Bi. Simba alieleza kuwa Wakala wa Vipimo umeshiriki maonesho ya Sabasaba tangu Juni 28 hadi Julai 13, na mafanikio ya kushiriki kwao mwaka huu yamekuwa makubwa zaidi ya matarajio yao kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi waliotembelea banda lao kwa lengo la kupata elimu.

"Jukumu letu kama WMA ni kuhakikisha vipimo vinavyotumika kwenye sekta mbalimbali vinazingatia usahihi unaotakiwa, ili mlaji apate kile kinachostahili," alisisitiza.

Alitolea mfano wa bidhaa zinazofungashwa kama sukari, kahawa, mafuta ya kupikia au bidhaa yoyote yenye alama ya uzito au ujazo, akisisitiza kuwa WMA hukagua kuhakikisha kinachodaiwa kipo kwenye kifungashio ndicho kilichopo kweli.

Pia alibainisha kuwa mizani ya kwenye bucha, ambayo ni ya kupimia nyama na bidhaa nyingine, huhakikiwa na WMA na hutambulika kwa kuwekwa stika maalum ya uthibitisho baada ya ukaguzi.

Kwa mujibu wa Bi. Simba, sekta nyingine zinazoguswa na vipimo ni pamoja na kilimo, afya na usafirishaji. Alieleza kuwa mizani ya kupimia mazao kama korosho na pamba pia hukaguliwa ili kuhakikisha wauzaji na wanunuzi wote wananufaika kwa usawa.

Katika Sekta ya Afya, alieleza kuwa ni muhimu kuhakikisha mizani inayotumika hospitalini kupima uzito wa wagonjwa ni sahihi kwani matibabu mengi hutegemea uzito sahihi wa mgonjwa.

Aidha, alibainisha kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa elimu ya vipimo, WMA imeandaa mikakati ya kuifikisha elimu hiyo kwa jamii kwa upana zaidi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha klabu mashuleni zitakazosaidia watoto kujifunza kuhusu vipimo na kujenga uelewa tangu wakiwa wadogo.

Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Temeke, Hilolimus Mahundi, aliwahimiza wananchi wanaonunua gesi ya kupikia kuhakikisha mtungi unapimwa kwenye mzani uliothibitishwa kabla ya kuondoka nao nyumbani.

 "Kabla ya kuondoka na mtungi wa gesi, hakikisha umeupima na ukibaini kuna tatizo, fika ofisi zetu zilizopo kila mkoa kwa msaada wa kisheria," alisema Mahundi.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.