TUME YAVIHIMIZA VYOMBO VYA HABARI KURIPOTI KWA USAHIHI HABARI ZA UCHAGUZI


Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinatoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwajibikaji kuhusu masuala yote yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza leo tarehe 1 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kidemokrasia, hasa kwa kutoa elimu ya mpiga kura.

“Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kusaidia kuwapa wananchi taarifa sahihi zitakazowasaidia kufanya maamuzi ya msingi kwa uhuru, amani na utulivu,” amesema Jaji Mwambegele wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Aidha, Jaji Mwambegele amewahimiza wahariri kuhakikisha wanatumia majukwaa yao kuwahamasisha wananchi waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani, akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, amesema vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa jukumu la Tume kufikisha elimu na taarifa kwa umma.


“Bila vyombo vya habari, juhudi zote za Tume haziwezi kufanikishwa. Kila taarifa inayotolewa na Tume haina maana yoyote kama haitafikishwa kwa wananchi kupitia ninyi,” ameeleza Bw. Kailima.


Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinao wajibu wa kuwa chanzo cha kwanza cha kupinga na kukanusha taarifa za upotoshaji zinazoweza kusambaa kwa makusudi au bahati mbaya kuhusu shughuli za uchaguzi.


“Tunahimiza kuwepo kwa taarifa za mara kwa mara zinazotoa hali halisi ya maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi ili kuwapa wananchi uelewa sahihi,” amesema.


Katika kikao hicho, wahariri wamekumbushwa pia kutumia kaulimbiu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 isemayo: “Kura Yako Haki Yako – Jitokeze Kupiga Kura” katika taarifa zao kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi.



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.