Na Mwandishi Wetu,
New York.
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa mwito wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuvutia wawekezaji kutoka Marekani.
Dk Mpango alisema hayo juzi katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).
Amesema ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ni nguzo muhimu ya kufungua fursa kubwa za kiuchumi nchini, huku akibainisha kuwa Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 185 kwa miaka mitano ijayo.
“Sekta binafsi ni mshirika muhimu katika jitihada zetu za maendeleo,” alisema, akifafanua kuwa Tanzania imefanya maboresho ya mfumo wa uwekezaji ili kuunda mazingira rafiki zaidi kwa PPP kwenye sekta za nishati, usafirishaji, afya na kidijitali.
Akitaja fursa za uwekezaji, Dk Mpango alisema Tanzania inatekeleza mradi wa reli ya kisasa ya kilometa 2,561 unaofadhiliwa kupitia PPP, utakaounganisha nchi na masoko ya kikanda yenye watumiaji zaidi ya milioni 300.
Aidha, alieleza kuwa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZs) yaliyounganishwa na bandari na kuendeshwa kwa nishati mbadala yapo tayari kwa uwekezaji wa pamoja. Pia, alitaja fursa katika sekta ya madini ya grafiti, nikeli na lithiamu, ambapo Tanzania inataka ushirikiano si tu katika uchimbaji, bali pia katika kuongeza thamani kupitia usindikaji na viwanda vya nishati safi.
Katika sekta ya kidijitali, Dk Mpango alisema Tanzania tayari imeanza ushirikiano na kampuni ya Visa kupitia kituo cha ubunifu Dar es Salaam, na kwamba teknolojia kama akili bandia (AI) na matumizi ya ndege zisizo na rubani zinaweza kuimarisha kilimo cha kisasa na minyororo ya thamani.
Makamu wa Rais alisema Serikali imefanya mageuzi makubwa ya uwekezaji, ikiwemo kupunguza muda wa usajili wa biashara kutoka siku 14 hadi saa 24 na kutoa vibali ndani ya saa chache kupitia kituo cha huduma kwa wawekezaji.
Pia, alisema Tanzania inaendelea kuwekeza katika elimu na ukuzaji wa ujuzi, huku ikijivunia utulivu wa kisiasa wa zaidi ya miaka 60 na faida kubwa kwa kampuni zinazowekeza, kati ya asilimia 20 hadi 30.
Akigusia Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA), Dk Mpango alisisitiza umuhimu wa kuhuishwa kwake kwa manufaa ya Marekani na Afrika kwa ujumla.
Alimalizia kwa kuwataka wawekezaji wa Marekani kuchukua hatua haraka, akionya kuwa washindani kutoka kanda nyingine tayari wanajipenyeza.



Hakuna maoni: