HESLB YACHANGIA MILIONI 10 KWA TEMEKE SEKONDARI KUBORESHA MASOMO YA SAYANSI


DAR ES SALAAM.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa msaada wa shilingi milioni kumi kwa Shule ya Sekondari Temeke jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara, lengo likiwa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono somo la sayansi.

“Taifa letu haliwezi kupiga hatua bila kuwa na wanasayansi. Tunaamini vifaa hivi vitawasaidia wanafunzi wa sayansi kusoma na kufanya mazoezi kwa vitendo,” alisema Dkt. Kiwia.

Aidha, Dkt. Kiwia alibainisha kuwa serikali ya awamu ya sita kila mwaka inafadhili zaidi ya wanafunzi 1,000 wa masomo ya sayansi kupitia Samia Scholarship ili kuongeza wataalamu wa fani hiyo nchini. Aliongeza kuwa tangu kuingia madarakani, serikali imetumia zaidi ya trilioni 1 kuwezesha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Ingia Mtenga, aliishukuru HESLB kwa msaada huo, akisema utasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa vifaa vya maabara.

Amesema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 2,637 (wavulana 1,321 na wasichana 1,310) imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kujifunzia, na msaada huo utakuwa chachu ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi, hasa katika masomo ya sayansi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.