SERIKALI YA HUNGARY YAFUNGUA RASMI OFISI ZA UBALOZI NCHINI TANZANIA, YASAINI MIKATABA YA MAENDELEO KATIKA NYANJA MBALIMBALI
Dar es Salaam, Septemba 29, 2025
Serikali ya Hungary imefungua rasmi Ofisi ya Ubalozi wake jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua kubwa ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Hungary na Tanzania.
Hatua hiyo ilitanguliwa na utiaji saini wa mikataba mbalimbali baina ya nchi hizo mbili, ikiwemo sekta za maji, biashara, elimu, kilimo na ushirikiano na sekta binafsi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo alimpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó kwa hatua hiyo, akieleza kuwa ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kihistoria na wa kimkakati kati ya mataifa haya mawili."Ufunguzi wa ofisi za ubalozi wa Hungary hapa nchini ni heshima kwa Tanzania. Hatua hii itaongeza fursa za uwekezaji, biashara, utalii na ushirikiano wa moja kwa moja baina ya wananchi wa nchi zetu mbili," alisema Balozi Kombo.
Mkataba wa Mradi Mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria
Miongoni mwa mikataba muhimu iliyosainiwa ni ule wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa usambazaji wa maji safi kutoka Ziwa Victoria hadi Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera. Mradi huo una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 55 na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 200,000.
Mikataba Mingine: Biashara, Elimu, Kilimo na Sekta Binafsi
Mbali na sekta ya maji, Tanzania na Hungary zimesaini pia mikataba ya ushirikiano katika maeneo ya:
Biashara – Kukuza uhusiano wa kibiashara na kuwezesha wawekezaji wa pande zote mbili.
Elimu – Kupanua fursa za elimu ya juu na mafunzo ya kitaaluma kwa vijana wa Tanzania.
Kilimo – Kushirikiana katika teknolojia za kilimo bora na usindikaji wa mazao.
Sekta binafsi – Mkataba maalum umesainiwa baina ya Hungary na sekta binafsi ya Tanzania, wenye lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kutumia uzoefu wa sekta binafsi.
Waziri Kombo alibainisha kuwa ushirikiano huu unakwenda sambamba na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha huduma za kijamii kwa wananchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó, alisema kuwa moja ya changamoto kubwa zinazozikabili nchi nyingi barani Afrika ni upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi. Alieleza kuwa kutokana na changamoto hiyo, Hungary imeona umuhimu wa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya maji, ikiwemo ule wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria, ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanafikiwa na huduma hiyo ya msingi.“Changamoto ya upatikanaji wa maji safi ni ya msingi barani Afrika. Kama Hungary, tumeamua kushirikiana na Tanzania kwa sababu tunaamini kuwa kupitia teknolojia na uzoefu tulionao, tunaweza kusaidia kuwafikia maelfu ya watu wanaohitaji huduma hii muhimu,” alisema Mhe. Szijjártó.






Hakuna maoni: