DAR ES SALAAM.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa mvua za Vuli (Oktoba–Disemba 2025) zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya nchi, zikitarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 11 Septemba 2025 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba 2025 katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Kigoma. Aidha, mvua hizo zitasambaa hadi pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba 2025, na zinatarajiwa kuisha Januari 2026.
Dkt. Chang’a alitoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, na mwezi pamoja na tahadhari zinazotolewa na TMA, akibainisha kuwa mwelekeo wa msimu unaotolewa ni wa miezi mitatu, hivyo kuna umuhimu wa kuzingatia viashiria vya muda mfupi na wa kati.
“Mvua za Vuli zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Desemba 2025, huku msimu huu ukitarajiwa kuwa na vipindi vya joto kali kuliko kawaida,” aliongeza.
Aidha, alisema TMA imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya, ambapo wilaya 86 zilizopo kwenye ukanda unaopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka zitapatiwa utabiri wa maeneo mahususi.
Msimu wa mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa Morogoro, Pwani ikiwemo Mafia, Dar es Salaam, Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) na kaskazini mwa Kigoma.
Hakuna maoni: