MOROGORO.
Viongozi na Makamanda wa Vituo vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametakiwa kuweka uwiano wa maisha ya kazi na binafsi na kutenga muda kwa familia na jamii ili kujiepusha na msongo wa mawazo unaoweza kusababisha matatizo ya afya ya akili.
Wito huo umetolewa Leo Februari 20, 2026 na Mtaalam wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka, wakati akitoa elimu ya afya ya akili katika siku ya tatu ya Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya TFS unaoendelea katika Ukumbi wa Hoteli ya Cate, Morogoro.
Dkt. Kweka alisema tafiti za afya ya akili zinaonyesha kuwa changamoto kubwa zinazochangia watu kupoteza maisha kwa kujiua zinahusishwa na mahusiano mabovu au hafifu na familia na jamii, hali inayoweza kusababisha maamuzi yasiyo sahihi.
“Ni muhimu kutenga muda kwa ajili ya familia na jamii. Mahusiano mazuri ni kinga dhidi ya msongo wa mawazo,” alisema.
Alisisitiza kuwa afya ya akili inahusisha uwezo wa mtu kudhibiti hisia na tabia zake, na kwamba kukosekana kwa uwiano kati ya kazi na maisha binafsi kunaweza kuathiri hali hiyo.
Misitu na utulivu wa akili
Akihusisha taaluma yake na wajibu wa TFS, Dkt. Kweka alisema misitu ina mchango mkubwa katika kuleta utulivu wa akili kwa binadamu, akieleza kuwa maeneo ya asili kama misitu na bahari husaidia kupunguza mihemko na msongo wa mawazo.
“Misitu ni utajiri, lakini utajiri wa kwanza wa mwanadamu ni afya yake. Ukilinda misitu, unalinda afya ya akili,” alisema.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira yanapoendelea, dunia inapoteza maeneo ya utulivu ambayo ni muhimu kwa ustawi wa binadamu.
Magonjwa sugu na mtindo wa Maisha
Mbali na afya ya akili, mtaalam huyo alizungumzia pia magonjwa sugu yanayoambukiza na yasiyoambukiza, akihimiza watumishi kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo kula kwa kiasi, kufanya mazoezi mara kwa mara, kunywa maji ya kutosha na kupunguza msongamano wa mawazo.
Alipongeza juhudi za TFS kuandaa bonanza la michezo kwa watumishi wake, akisema mazoezi ni nyenzo muhimu ya kulinda afya ya mwili na akili, hasa kwa taasisi yenye majukumu ya kiulinzi kama TFS.
Wito kwa Watanzania
Dkt. Kweka aliwataka Watanzania kuendelea kulinda misitu, akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira unachangia si tu uchumi na hali ya hewa, bali pia afya ya akili ya jamii.
“Tusikate miti bila kupanda. Tukilinda misitu, tunalinda afya yetu ya leo na ya kesho,” alisema.
Mkutano huo wa viongozi wa TFS unaendelea kujadili masuala ya utendaji, ustawi wa watumishi na mikakati ya kuimarisha uhifadhi wa misitu nchini.







Hakuna maoni: