JAB YAMPA ONYO KALI MWANDISHI WA HABARI ZUNGU KWA KUTOA LUGHA ISIYO NA STAHA KUHUSU TUKIO LA NDEGE YA ATCL KUCHELEWA


Dar es Salaam, Februari 23, 2026.

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imempa onyo kali mwandishi wa habari Bw. Kelvin Justine Raphael, maarufu kwa jina la Zungu (Matejoo), kwa kukiuka maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika maudhui aliyoyachapisha kuhusu tukio la uchelewaji wa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Kwa mujibu wa taarifa ya JAB, mwandishi huyo alitumia lugha isiyo ya staha, ikiwemo matusi na kejeli, hali iliyokiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari na kuathiri taswira ya taaluma hiyo pamoja na heshima inayopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa taarifa kwa umma. 

Bodi ilimwita na kumpa fursa ya kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu, ambapo ilijiridhisha bila shaka kuwa alikiuka kanuni na maadili ya uandishi wa habari. 

Katika hatua iliyofuata, mwandishi huyo alikiri makosa yake na kuomba radhi, ambapo JAB imemtaka kuondoa mara moja maudhui aliyoyachapisha kwenye majukwaa yote ya mitandao ya kijamii, kuacha tabia hiyo, na kurejea katika misingi ya weledi, uwajibikaji na maadili ya taaluma. 

Aidha, Bodi imemwonya kuwa endapo atarudia au kuendelea na vitendo vya aina hiyo, haitasita kuchukua hatua kali zaidi za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kusimamisha au kufuta ithibati yake kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023). 

JAB imewakumbusha waandishi wote wa habari kuwa uhuru wa kujieleza hauondoi wajibu wa kuzingatia maadili ya taaluma, na kwamba uandishi wa habari ni nguzo muhimu ya jamii unaopaswa kuendeshwa kwa weledi, ukweli, uwiano na matumizi ya lugha yenye staha ili kulinda heshima na uaminifu wa taaluma hiyo nchini. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.