Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mwanamitindo maarufu wa kimataifa, Miriam Odemba, leo ameungana na watoto wa Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu ambayo inahudumia watoto wenye ulemavu jijini Dar es Salaam kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, hatua iliyoonyesha upendo na moyo wa kujitoa kwa jamii.
Odemba ametimiza umri wa miaka 44, ambapo alianza safari yake ya uanamitindo akiwa na umri wa miaka 14, na tangu wakati huo amekuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengi ndani na nje ya Tanzania.
Mtoto Rahma Omary, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, amemshukuru Odemba kwa kuwakumbuka na kusherehekea nao katika siku yake ya kumbukizi ya kuzaliwa, akisema hatua hiyo imewapa furaha na matumaini makubwa.
Akizungumza kwa njia ya mtandao akiwa nje ya Tanzania, Miriam Odemba amesema amefurahishwa kuona watoto hao wakifurahia siku hiyo pamoja naye. Ameeleza kuwa anawapenda sana watoto hao na kuahidi kuwa atakaporejea nchini atakutana nao ana kwa ana na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Ameongeza kuwa ulemavu sio kikwazo cha wao kutimiza ndoto na malengo yao, akisisitiza kuwa watoto hao wana uwezo wa kufanya mambo makubwa yatakayoshangaza dunia endapo watapata msaada na mazingira rafiki.
Kaimu Mkuu wa Shule hiyo amesema kutokana na mchango wake chanya kwa jamii, hususan katika shule hiyo ambako amekuwa akiwatembelea mara kwa mara na kutoa misaada, uongozi wa shule umemtunuku tuzo maalumu ya kutambua mchango wake kwa jamii. Aidha, wameeleza shukrani zao kwa msaada mkubwa alioutoa.
Kupitia Taasisi ya Miriam Odemba Foundation, zilitolewa zawadi mbalimbali ikiwemo sukari, unga, mchele, maharage, sabuni, nepi (diapers) na mahitaji mengine muhimu kwa watoto wa shule hiyo.
Katika sherehe hiyo, wawakilishi wa Miriam Odemba walikata keki ya siku ya kuzaliwa na kupata chakula cha jioni pamoja na watoto hao, huku wakiahidi kuendelea kuwatembelea mara kwa mara na kusaidia mahitaji ya shule hiyo.
Mama wa Miriam Odemba aliwasilisha salamu za upendo na baraka kwa watoto hao, akiwatakia heri na mafanikio katika masomo na maisha yao ya baadaye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Miriam Odemba, Jenifa Mteleki, amesema maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Odemba ni sehemu ya kurejesha kwa jamii, akieleza kuwa taasisi hiyo imefurahi kuona wanagusa maisha ya watoto wenye uhitaji.
“Kama taasisi tumeona ni vyema kushirikiana na shule hii kwa kile Mungu alichotubariki. Kundi hili limekuwa likisahaulika katika jamii, hivyo tunatoa rai kwa jamii kujitokeza kuwasaidia yatima, wajane, walemavu na wenye uhitaji ili kupata baraka za Mungu,” amesema Mteleki.
Matroni wa shule hiyo, Capt. Consolata Magesa, amesema Miriam Odemba amekuwa akiwashika mkono mara kwa mara na kwamba sherehe hiyo imekuwa baraka kubwa kwa shule hiyo. Ameongeza kuwa shule inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa mahitaji ya msingi, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kusaidia.Sherehe hiyo imeacha ujumbe mkubwa kwa jamii kuhusu umuhimu wa upendo, mshikamano na kuwajali watu wenye mahitaji maalumu, huku Miriam Odemba akiendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kutumia umaarufu wake kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.












Hakuna maoni: