DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya uzinduzi rasmi wa Soko la Kariakoo Februari 8, 2026, kufuatia kukamilika kwa mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko jipya baada ya soko la awali kuathiriwa na ajali ya moto.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema ujenzi wa soko hilo umefikia hatua ya mwisho kwa asilimia 100, huku serikali ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 28 kugharamia mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Chalamila amesema soko hilo jipya lina miundombinu ya kisasa na lina zaidi ya vizimba 1,500 vitakavyowawezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kufanya biashara zao katika mazingira salama na yenye uhakika wa kudumu.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na wafanyabiashara kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo muhimu, akieleza kuwa tukio hilo ni fursa ya kumuunga mkono Rais Samia na kuandika historia mpya ya maendeleo ya biashara katika Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza wafanyabiashara wadogo waliovamia na kufunga njia za kuingia sokoni kuondoa shughuli zao mara moja na kuziacha barabara wazi kabla ya Februari 8, ili kuruhusu upatikanaji rahisi wa soko hilo na kuimarisha usalama pamoja na mpangilio wa shughuli za biashara.

Hakuna maoni: