Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne Muliro, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na vitendo vya kihalifu, huku akiwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama jijini Dar es Salaam ni shwari.
Amesema jeshi hilo linaendelea kuwahimiza wananchi kutoa taarifa muhimu zinazosaidia kudhibiti uhalifu, hatua inayochangia kulinda amani na usalama wa jiji hilo.
Katika kipindi cha kuanzia Januari 30 hadi Februari 24, 2026, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata jumla ya watuhumiwa 46 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya kijinai.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam, SACP Muliro amesema miongoni mwa makosa yaliyobainika ni unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji wa nyumba na maghala (godown), pamoja na wizi wa mali za umma na binafsi.
Amebainisha kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitumia pikipiki na silaha za jadi kama vile mapanga kutekeleza uhalifu, hususan katika maeneo ya pembezoni mwa jiji.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakijihusisha na kuvunja nyumba mchana na usiku na kuiba vifaa mbalimbali, huku wengine wakihusika na kununua na kuuza mali za wizi.
“Jeshi la Polisi limekamata pikipiki zaidi ya 20, simu 110, runinga, redio na vifaa vingine vya kielektroniki. Pia zimekamatwa funguo maalum zenye uwezo wa kufungua kufuli za aina mbalimbali pamoja na gari lenye namba ya usajili T 457 CQF aina ya Toyota Noah lililokuwa likitumika kusafirisha mali za wizi,” amesema Muliro.
Ameongeza kuwa miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni Rashidi Mtunguja maarufu “Msamba” na wenzake wanne waliokamatwa maeneo ya Jangwani, Issa Nasoro Kurukutu na wenzake wawili waliokamatwa Gongo la Mboto, pamoja na Nicholas Abdallah Said mkazi wa Manzese.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa ufuatiliaji unaendelea ili kuwakamata wahusika wote kabla au baada ya kutekeleza uhalifu, sambamba na kukusanya ushahidi ili kuwafikisha katika Ofisi ya Mashitaka na hatimaye mahakamani.
Katika hatua za kisheria zilizochukuliwa, SACP Muliro amesema baadhi ya watuhumiwa wamehukumiwa vifungo vikali ikiwemo kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ubakaji wa kundi na unyang’anyi wa kutumia silaha. Miongoni mwao ni Mwita Marwa na wenzake wawili waliopatikana na hatia katika Mahakama ya Kigamboni, Adam Samiro aliyehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, pamoja na Jafari wa Chang’ombe na Omari Omari wa Mbande waliopata adhabu kali katika Mahakama ya Temeke.
Kwa upande wa usalama barabarani, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, hususani wanaopita kwenye barabara za mwendo kasi. Jumla ya madereva 250 walikamatwa katika kipindi hicho, wakiwemo bodaboda 167, bajaji 19 na magari 64, hatua iliyolenga kupunguza ajali na kero kwa watumiaji wa barabara.
Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na kuahidi kuendelea kulinda usalama ili shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani.
Pamoja na hayo, Kamanda Muliro akiwa pamoja na waandishi wa habari, amefanya ziara katika Soko la Kariakoo na kushuhudia utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha njia za kuingia na kutoka katika soko hilo kuu zinapitika.
Katika ziara hiyo, Kamanda Muliro amesema agizo hilo limetekelezwa kikamilifu kwa kuondolewa kwa wamachinga waliokuwa wamesonga njia hizo, na kueleza kuwa utekelezaji huo umefanikiwa kwa asilimia 100, hatua inayolenga kurahisisha shughuli za kibiashara na kuongeza usalama kwa wafanyabiashara na wananchi wanaotumia soko hilo.


Hakuna maoni: