SERIKALI YAENDELEA KUONGEZA THAMANI NA KUBORESHA MASOKO YA DHAHABU GEITA


Na Wizara ya Madini, 

Dodoma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha uongezaji thamani madini katika Mkoa wa Geita ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali madini yanabaki nchini.

 Dkt.Kiruswa amesema hayo leo Februari 06, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe.Eng.Chacha Mwita Wambura aliyetaka kufahamu ni lini kitaanzishwa Kituo cha kuongeza thamani na soko la bidhaa za dhahabu katika Mji wa Geita.

Amesema Kutokana na uzalishaji mkubwa wa dhahabu, mkoa wa Geita umewekewa miundo mbinu muhimu ikiwemo viwanda vikubwa vya Kusafisha Dhahabu vya Geita Gold Refinery (GGR) na African Eyes Refinary, viwanda vidogo vya teknolojia ya kisasa ya kuchakata dhahabu (CIP/CIL) pamoja na vituo vya mfano vya Lwangasa na Katente vinavyosimamiwa na Shirika la madini la Taifa (STAMICO ), “Kuwepo kwa hatua hizi na kwa kuzingatia Sheria na Sera zilizopo, zimefungua fursa kwa wadau mbalimbali kushiriki katika soko la bidhaa za dhahabu Mjini Geita ikiwepo masuala ya usonara,” amesema Dkt. Kiruswa.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kiujuzi, kiuwekezaji na kisheria ili kuimarisha uongezaji thamani madini nchini, na kufanya shughuli za madini ziendelee kuleta manufaa kwa jamii na serikali kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Wizara kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) inaendelea kutoa mafunzo ya vitendo ya uongezaji thamani madini na kuandaa wataalam wa utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na dhahabu, fedha na vito, ambapo amemuomba Mhe. Mbunge kuhamasisha vijana Mkoani Geita kuchangamkia fursa hizo ili waweze kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia shughuli za madini kwenye maeneo yao.


#LocalContent

#MadininiMaisha&Utajiri

#Kutoka Bungeni

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.