Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ametembelea miradi ya ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo Sinza Simu 2000, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga takribani shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TMA, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utoaji wa taarifa sahihi na za uhakika za hali ya hewa nchini.
Ameeleza kuwa miradi hiyo inahusisha ujenzi wa jengo la kisasa la Kanda ya Mashariki na Kituo cha Utoaji Tahadhari za Hali ya Hewa pamoja na Kituo cha Tahadhari za Tsunami, sambamba na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa Vifaa vya Hali ya Hewa (National Meteorological Calibration Centre), kitakachosaidia kukagua na kuboresha usahihi wa vifaa vya hali ya hewa.
Mhe. Kihenzile amesema majengo hayo, yaliyoanza kujengwa mwaka 2023 na 2025, yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, na kwamba kukamilika kwake kutawawezesha wataalamu wa TMA kufanya kazi katika mazingira bora na ya kisasa, hivyo kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa kwa wananchi.
Kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, ametoa wito kwa Bodi na Menejimenti ya TMA kusimamia miradi hiyo kwa weledi, uzalendo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa. Aidha, ameipongeza TMA kwa kumchagua mkandarasi wa ndani, Chuo cha DIT (Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam), kutekeleza miradi hiyo, akisema hatua hiyo inachochea maendeleo ya wataalamu na taasisi za ndani.
Vilevile, Naibu Waziri amesisitiza umuhimu wa TMA kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili kuwasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali zikiwemo usafiri, kilimo na shughuli za baharini, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kuamini na kutumia taarifa rasmi zinazotolewa na TMA.



Hakuna maoni: