DAR ES SALAAM.
Said Nestory Mwaipopo amezindua rasmi mfuko maalum wa kusaidia wahitaji katika jamii, akilenga kuimarisha ustawi wa makundi yaliyo katika mazingira magumu na kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wananchi. Uzinduzi huo umefanyika mbele ya waumini na wadau mbalimbali waliokusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu ya kijamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Sheikh Mwaipopo amesema mfuko huo unalenga kutoa msaada wa haraka na wa muda mrefu kwa watu wasiojiweza, huku akitoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi kuchangia kuanzia shilingi 2,000 ili kufanikisha azma hiyo. Amesema kila mchango, mdogo au mkubwa, una thamani katika kubadili maisha ya wahitaji.
Ameeleza kuwa makundi yatakayonufaika na mfuko huo ni pamoja na watoto yatima, wajane, wazee wasiojiweza, watu wenye ulemavu pamoja na familia zenye changamoto za kipato. Lengo ni kuhakikisha wanapata msaada wa mahitaji muhimu kama chakula, mavazi, huduma za afya na elimu.
Kwa mujibu wake, mfuko huo utasimamiwa kwa uwazi na uadilifu ili kuhakikisha rasilimali zitakazokusanywa zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya walengwa. Ameongeza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali utakuwa chachu ya mafanikio ya mpango huo.
Sheikh Mwaipopo amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa mshikamano, upendo na huruma katika kujenga jamii imara, akisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika kusaidia wenye uhitaji na kuleta matumaini mapya kwa makundi yaliyo katika changamoto.

Hakuna maoni: