TMA YATOA MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA 2026, YAONYA MAFURIKO NA UPUNGUFU WA MAJI


DAR ES SALAAM. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika kwa mwaka 2026, ikieleza kuwa baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani huku mengine yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Akizungumza na Waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo mapema hii leo Februari 5, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a amesema mvua za Masika zinatarajiwa kunyesha katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2026, hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ikiwemo Ukanda wa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Dkt. Chang'a amesema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Pwani ya Kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya magharibi mwa Ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo mikoa ya Kagera na Geita pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.

Kwa upande wa mwanzo wa msimu, mvua za Masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Februari hadi wiki ya kwanza ya Machi katika Ukanda wa Ziwa Victoria, huku maeneo ya Pwani ya Kaskazini yakitarajiwa kuanza kupokea mvua kuanzia wiki ya kwanza hadi ya pili ya Machi. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya Mei na wiki ya kwanza ya Juni, 2026.

Aidha ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Aprili, hali ambayo inaweza kusababisha vipindi vya unyevu kupita kiasi na mafuriko katika baadhi ya maeneo, hali inayoweza kuathiri shughuli za kilimo, miundombinu na makazi ya watu.

TMA imeonya kuwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi za maji ardhini kinaweza kupungua, jambo linaloweza kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu, mifugo na kilimo.

Pia, mamlaka hiyo imesema magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa vyanzo vya maji hasa katika maeneo yatakayokumbwa na mvua nyingi na mafuriko.

Kutokana na hali hiyo, TMA imewataka wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, afya, nishati, maji, ujenzi, usafiri pamoja na menejimenti za maafa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza shughuli zao.

TMA imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi na taasisi kufuatilia utabiri wa kila siku, wa siku kumi na wa kila mwezi pamoja na tahadhari zinazotolewa rasmi na mamlaka hiyo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.