Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amefungua rasmi mafunzo ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) yanayolenga kuongeza ufanisi, uwajibikaji na tija kwa watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Februari 16, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini Dodoma, Mbibo amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea uwezo watumishi ili kuboresha utendaji wao wa kila siku, hatua itakayochochea utekelezaji wenye mafanikio wa majukumu ya Wizara.
Amesisitiza kuwa mafunzo ya ESG yanatoa msingi mpana wa kufanya kazi kwa kuzingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira, ustawi wa jamii na misingi ya utawala bora, hivyo kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya utendaji.
Mbibo amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo, akibainisha kuwa maarifa yatakayopatikana yataongeza ufanisi binafsi na wa taasisi kwa ujumla, pamoja na kuwawezesha washiriki kuwashirikisha na kuwaelimisha wenzao katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, amewapongeza waandaaji wa mafunzo hayo ambao ni Idara ya Uhasibu kwa kushirikiana na Kitengo cha Tehama, akitoa wito wa kuendelea kuandaa mafunzo ya aina hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuboresha utendaji wa watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Muhasibu kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na mkufunzi wa mafunzo hayo, Steven Mrema, amesema mafunzo ya ESG yamejikita katika kuwawezesha washiriki kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya mazingira endelevu, uwajibikaji wa kijamii na utawala bora, sambamba na kuzingatia sera na miongozo ya Serikali.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku 14, ambapo washiriki watapata mafunzo ya kina kuhusu maeneo mbalimbali wanayopaswa kuyafanyia kazi katika vitengo vyao ili kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.



Hakuna maoni: