WAZIRI NDEJEMBI AKABIDHI MAGARI KWA MAMENEJA WA TANESCO - TABORA

 


TABORA.

Waziri wa nishati Mhe. Deogratius Ndejembi Februari 14, 2026 amekabidhi vitendea kazi vya usafiri kwa mameneja wa TANESCO wa Wilaya za Skonge, Urambo na Igunga Mkoani Tabora ili kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi na kutatua changamoto zao kwa wakati.

Akizungumza wakati akikabidhi magari hayo kwa Meneja wa TANESCO wilayani Urambo kwa niaba ya wengine, Januari 14, 2026 Mhe. Ndejembi amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Bw. Lazaro Twange kwa kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kuhakikisha mwananchi anafikiwa bila kujali mazingira aliyopo.

Amesema hatua hiyo ya kununua vitendea kazi ni kuyaishi maono ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya utendaji kazi katika Mashirika ya umma ambapo TANESCO imeonesha mfano na sasa wateja takribani milioni 5.6 watapata umeme wa uhakika na kuhudumiwa kwa wakati. 

‘’Ninatamani kuona mnafanya mabadiliko makubwa katika kumfikia mteja kwa haraka, eneo la kumsikiliza na kumuhudumia mteja tunafanya vizuri sana, sasa tukaongeze nguvu ya kutatua changamoto za wateja kwa wakati kwa kutumia vyombo hivi vya usafiri’’ alifafanua Mhe. Ndejembi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema mpaka sasa TANESCO imepokea magari 120 yakiwemo malori na magari madogo hatua hiyo imelenga kuhakikisha mwananchi anahudumiwa kwa ufanisi.

‘’Mpaka sasa tumepokea magari 120 , yakiwemo malori, magari mengine 12 makubwa ya crane yako bandarini, hivi karibuni tulipokea magari 51 kwa lengo la kusambaza katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa huu wa Tabora ambao mpaka sasa tumeshaleta magari matano’’ alisisitiza Bw. Twange.

TANESCO imeendelea kufanya jitihada za kununua vitendea kazi vya usafiri, yakiwemo magari madogo, malori bajaji na pikipiki, ili kuhakikisha wateja wanafikiwa na kutatuliwa changamoto zao kwa haraka.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.