BOLT YAKUTANA NA LATRA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA UDHIBITI KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA MTANDAO


Dar es Salaam, 13 Machi 2026.

Kampuni ya Bolt Tanzania imekutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na wawakilishi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, katika kikao cha ngazi ya juu kilicholenga kujadili masuala muhimu ya udhibiti na uzingatiaji wa sheria katika sekta ya usafiri wa mtandao, pamoja na kutafuta suluhu za vitendo zitakazochochea ukuaji endelevu wa sekta hiyo.

Katika kikao hicho, Bolt iliwasilisha mkakati wake wa soko wa mwaka 2026, unaojumuisha mpango wa kuongeza idadi ya madereva na abiria kwa takribani asilimia 40, kuanza rasmi shughuli zake Zanzibar, pamoja na kupanua huduma katika miji mingine ya Tanzania Bara. Kampuni hiyo imeeleza kuwa kwa sasa inatoa huduma katika miji minane nchini, ikiwemo Mwanza, Morogoro, Mbeya na Tanga.

Aidha, Bolt imeeleza dhamira yake ya kuimarisha mfumo wa usafiri wa mtandao kwa kushirikiana kwa karibu na wadhibiti wa sekta ili kurahisisha upatikanaji wa leseni za kibiashara kwa madereva. Hatua hiyo inajumuisha mpango wa kampeni ya pamoja uitwao “Drive to Compliance”, utakaolenga kuongeza uelewa, kurahisisha mchakato wa urasimishaji na kuhamasisha madereva kushiriki katika sekta hiyo kwa njia salama na halali.

Akizungumza katika kikao hicho, Meneja Mkuu wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, alisema lengo la kampuni hiyo ni kuimarisha ushirikiano na wadhibiti ili kuchochea ukuaji wa sekta huku ikizingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

“Lengo letu ni kushirikiana kwa karibu na wadhibiti ili kufungua thamani katika mfumo mzima wa sekta. Ukuaji endelevu lazima uambatane na uzingatiaji wa sheria, haki na urasimishaji ulio thabiti,” alisema Kanyankole.

Kwa upande wake, Mkuu wa Udhibiti na Sera wa Bolt Afrika, Weyinmi Aghadiuno, alisema kikao hicho ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo katika kukuza uwazi na majadiliano yanayozingatia ushahidi.

“Ushirikiano wa kimfumo utaimarisha uadilifu wa udhibiti, kuhakikisha bei zinakuwa za haki na kurahisisha uendeshaji wa madereva katika maeneo yote tunakofanya kazi,” alieleza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa LATRA, Halima Lutavi, alisisitiza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kusawazisha udhibiti wa sekta ya usafiri na ubunifu wa teknolojia.

“LATRA iko tayari kwa majadiliano yenye tija yatakayolinda usalama, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kuhakikisha haki katika sekta, huku ikiunga mkono ubunifu,” alisema Lutavi.

Majadiliano katika kikao hicho pia yaligusia ujumuishaji wa mifumo ya kiteknolojia (API integration), upatikanaji wa uthibitishaji wa leseni kwa wakati halisi (TRI), upatikanaji wa maeneo ya biashara katikati ya jiji (CBD) kwa waendesha bodaboda, utekelezaji wa tozo za kisheria pamoja na mikakati ya kudhibiti safari zinazofanyika nje ya mfumo wa programu ili kuimarisha usalama na kulinda mapato ya serikali.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.