DAR ES SALAAM
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa wito kwa taasisi za umma, binafsi, na wafanyabiashara kote nchini kuhakikisha wanahakiki taarifa za kampuni na majina ya biashara kabla ya kuingia makubaliano yoyote ya kibiashara.
Katika taarifa iliyotolewa leo Machi 12, 2026, BRELA imebainisha kuwepo kwa baadhi ya kampuni zinazofanya biashara na kuingia mikataba bila kuhuisha taarifa zao au kufanya biashara ambazo hazijasajiliwa na Msajili wa Kampuni, jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria.
Msajili wa Kampuni amesisitiza kuwa usajili wa kampuni na majina ya biashara hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni (Sura ya 212) na Sheria ya Majina ya Biashara (Sura ya 213). Hivyo, ni muhimu kwa wadau wote kuhakikisha uhalali wa kampuni wanazofanya nazo kazi ili kuepuka changamoto za kisheria.
Huduma za uhakiki wa taarifa hizi zinapatikana kwa urahisi kupitia mfumo wa usajili wa njia ya mtandao (Online Registrations System - ORS) kupitia tovuti yao ya https://ors.brela.go.tz/ors/.
Kwa maelezo zaidi, wananchi wameshauriwa kuwasiliana na BRELA kupitia namba ya simu 0222212800 au kwa barua pepe maoni@brela.go.tz. Taarifa hii imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha wakala huo.


Hakuna maoni: