DAR ES SALAAM.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezitaka taasisi za umma na binafsi kushirikiana kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia, ili kuepuka madhara ya nishati chafu.
Amesema nishati safi, ikiwemo umeme, zinafaida lukuki ikiwemo gharama nafuu, usalama, na urahisi wa matumizi. Pia amesema Serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wanawake kutumia nishati safi, ili kulinda afya zao na mazingira.
Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam wakati akihutubia kwenye Kongamano la Pili la Wanawake wa TANESCO, lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall. Kongamano hilo linalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dkt. Gwajima amebainisha kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2022 zinaonyesha asilimia 81.5 ya kaya bado zinatumia kuni na mkaa kwa kupika, jambo linalosababisha changamoto za kiafya na uharibifu wa mazingira.
“Wanawake ndio waathirika wakuu wa nishati isiyo safi. Ni muhimu kuwapa elimu, mitaji na teknolojia rafiki zitakazowawezesha kutumia nishati safi kama umeme,” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesisitiza kuwa wanawake wanaheshimiwa ndani ya shirika na nafasi zao hazipuuziwi. Amehakikishia kuwa uongozi utaendelea kusimamia haki na maslahi yao kwa usawa wa kijinsia.
Twange pia alisisitiza mshikamano wa TANESCO na wanawake duniani katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, huku akibainisha kuwa shirika linaunga mkono juhudi za serikali, zikiongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhamasisha majiko ya umeme na kuachana na nishati zisizo salama.
Ameongeza kuwa TANESCO itashirikiana na wadau wote kuhakikisha ajenda ya nishati safi inatekelezwa kwa vitendo.


















Hakuna maoni: