FAINALI KABWILI CUP 2026 KUFANYIKA DAR, BINGWA KUJINYAKULIA GARI KUTOK KWA MDHAMINI MKUU NANASI GROUP

Na Mwandishi Wetu.

Macho na masikio ya mashabiki wa soka la mtaani jijini Dar es Salaam yataelekezwa Alhamis hii kwenye Uwanja wa Tabata Twiga, ambapo fainali za mashindano ya Kabwili Cup 2026 zinatarajiwa kupigwa kuanzia saa 2 usiku.

Mchezo huo wa mwisho utazikutanisha timu za Makuburi SC na Azimio FC, zote zikitokea maeneo ya Tabata, katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Akizungumza kuelekea kilele cha mashindano hayo, mratibu wa Kabwili Cup, Ramadhan Kabwilialiyewahi kuichezea Klabu ya Young Africans—amesema bingwa wa mwaka huu atajishindia gari, ikiwa ni zawadi ya kipekee inayolenga kuongeza hamasa kwa timu shiriki.

Mbali na zawadi hiyo kubwa, pia kutakuwa na tuzo mbalimbali kwa wachezaji waliofanya vizuri katika vipengele tofauti, huku mashabiki wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani hiyo.

Kabwili pia ametoa rai kwa wakazi wa Tabata, hususan eneo la Twiga, kutunza miundombinu ya uwanja huo ikiwemo taa zilizofungwa kwa udhamini wa kampuni ya Nanasi Group, ili ziendelee kusaidia michezo ya usiku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nanasi Group ameeleza kuwa kampuni hiyo imewekeza katika uwekaji wa taa za kisasa uwanjani hapo ili kuboresha mazingira ya michezo, na ameahidi kuendelea kushirikiana kuhakikisha fainali hiyo inafanikiwa. Aidha, amethibitisha kuwa kampuni yake ndiyo itakayotoa gari kwa mshindi wa michuano hiyo.

Ili kuhakikisha haki inatendeka uwanjani, waamuzi wenye beji za FIFA wanatarajiwa kusimamia mchezo huo, hatua inayoongeza hadhi ya mashindano hayo ambayo sasa yanafanyika kwa mwaka wa sita mfululizo.

Kabwili amesisitiza kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana, akieleza kuwa wengi wa wachezaji bora hutokea katika soka la mitaani, na kuwataka vijana kuendelea kujituma ili kufikia mafanikio.

Ratiba inaonesha kuwa shughuli zitaanza mapema saa 11 jioni kwa michezo ya watoto chini ya umri wa miaka 11, kabla ya pambano kuu la wakubwa kati ya Makuburi SC na Azimio FC kuanza saa 2 usiku.

Kocha wa Makuburi SC amewakaribisha mashabiki kujitokeza kwa wingi kuunga mkono soka la vijana, huku nahodha wa Azimio FC, Seseme, akiahidi ushindi na kumpongeza Kabwili kwa juhudi zake za kuendeleza mashindano hayo kwa miaka sita mfululizo.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.