KARATU YAONESHA NJIA: KILIMO IKOLOJIA CHAFUNGUA FURSA NA MASOKO MAPYA


Karatu, Arusha.

Wilaya ya Karatu inashuhudia ongezeko la wakulima wanaojikita katika kilimo ikolojia, mfumo unaolenga kulinda mazingira, kutoa mazao salama, na kuongeza kipato kwa wakulima.

Ziara maalumu iliyofanywa na waandishi wa habari chini ya shirika la Iles de Paix (IDP) katika maeneo ya Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, imeonesha taswira halisi ya mafanikio na changamoto za kilimo ikolojia.

Waandishi walipata fursa ya kutembelea mashamba ya wakulima wa kilimo ikolojia, kituo cha mafunzo, na miradi ya kuongeza thamani ya mazao, huku wakisikiliza uzoefu wa wakulima kuhusu mbinu za asili wanazotumia, faida wanazopata, na changamoto wanazokabiliana nazo.

Katika ziara hiyo, ilionekana wazi kuwa kilimo ikolojia si tu njia ya kulinda mazingira, bali pia ni fursa ya kiuchumi inayowawezesha wakulima kuongeza kipato na kuboresha afya ya waìlaji.


Kilimo Ikolojia kwa Ukubwa na uzalishaji Biogas na mbolea bora
Moja ya mifano ya mafanikio hayo inaonekana kwa Mzee George Ndege, mkulima kutoka kitongoji cha Ayalabe, ambaye amewekeza kwa kiwango kikubwa katika kilimo ikolojia. Analima kahawa kwenye hekta 10 na mboga za majani kwenye hekta moja, huku akitumia mbolea na viwatilifu vya asili.

Mbali na kilimo, ameanzisha mtambo wa biogas, unaomwezesha kuchakata samadi ya ng’ombe na mimea ili kupata gesi ya kupikia na mbolea safi kwa ajili ya mimea yake. Mazao yake, hususan mbogamboga, huuza kwa wingi kwenye hotel za kitalii, zinazothamini mazao yasiyo na kemikali.

“Kila mtu anapaswa kulima kilimo hai ili kutunza mazingira. Mbali na afya, pia kuna soko la uhakika,” anasema Mzee Ndege.

Mzee Ndege pia anafuga mifugo mbalimbali inayomwezesha kupata mbolea hizo za samadi anazotumia katika Shamba lake, mifugo hiyo ni pamoja na kuku,ng'ombe na Nyuki ambao wanasaidia kuchavusha kwenye mimea

Kupitia shughuli zake, ameweza pia kutoa ajira, akiwemo Patrick Sule, anayejifunza kilimo hai kwa vitendo na kujiandaa kuanzisha shamba lake mwenyewe.

Uzalishaji wa Viwatilifu na Mbole
Kwa upande wa uzalishaji wa pembejeo za kilimo, Adili Msangi, mkulima na mfugaji kutoka kijiji cha Bughari, ameonyesha mafanikio katika utengenezaji wa mbolea na viwatilifu vya asili kwa kutumia masalia ya wanyama na mimea.

“Mbolea na viwatilifu hivi vinatunza udongo, hupunguza asidi na kurejesha viumbe hai muhimu. Pia vinanipa kipato na kunirahisishia kufundisha wakulima wengine,” anasema Adili.

Kupitia shughuli zake, Adili amefanikiwa kufundisha wakulima katika mikoa zaidi ya 10, akichangia kueneza maarifa ya kilimo ikolojia nchini.

Benki ya mbegu asili
Ziara pia ilimkuta Mzee Modest Fantee kutoka kijiji cha Endagem, ambaye amejikita kikamilifu katika kilimo ikolojia cha mahindi, maharage na matunda mbalimbali. Anafanya kilimo hiki kwa kutumia mbegu na mbolea za asili, akisisitiza kuwa mazao yanayotokana na mbegu za asili yana virutubisho vya juu zaidi kuliko yale yanayotumia kemikali. Mzee Fantee pia anahifadhi mbegu asili katika “benki” ndogo ya mbegu, zinazosaidia wakulima wengine kupata mbegu salama na kuepuka upotevu.

“Tunatumia mbolea za samadi kutoka kwa wanyama na viwatilifu vya asili kama mwarobaini, aloe vera, na mkojo wa wanyama. Mazao haya yanashambuliwa kidogo tu, na ukitumia mbinu hizi za asili unaweza kukabiliana na wadudu na magonjwa haraka zaidi,” alisema Mzee Fantee.

Mbali na kuboresha mazao yake, Mzee Fantee amebaini kuwa kilimo ikolojia kina changamoto zake, ikiwemo kupata elimu ya kutosha kwa wakulima na ukosefu wa sera za kilimo ikolojia. Hata hivyo, ameendelea kueneza maarifa kwa wakulima wengine na kuonesha jinsi kilimo hai kinavyoweza kuwa chaguo la kiuchumi lenye tija kwa jamii.

Utengenezaji wa Vitafunwa vya Kilimo Hai
Kutoka kwenye uzalishaji mkubwa wa mazao, ziara ilielekea pia kwenye upande wa uongezaji thamani, ambapo Stella Marick, mjasiriamali kutoka kijiji cha Bashay, anatumia mazao ya kilimo ikolojia kutengeneza mikate, keki na clips.

“Tunajali afya ya walaji wetu, ndiyo maana tunatumia mazao ya kiikolojia,” anasema Stella.

Biashara yake imeweza kutoa ajira 12 za moja kwa moja, huku wengine wakinufaika kupitia usambazaji na uuzaji. Hata hivyo, anakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, inayokwaza uzalishaji.

Kauli ya Serikali kupitia viongozi wa Wilaya.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, viongozi wa ngazi ya wilaya wameahidi kuendelea kusimamia na kuhamasisha maendeleo ya kilimo ikolojia ili kuwainua wakulima na kulinda mazingira.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu,Engelbert Qorro amesema kilimo ikolojia kina mchango mkubwa katika kuwaunganisha wakulima na masoko, hususan sekta ya utalii.

“Kilimo hiki kinatoa fursa kubwa kwa wakulima wetu kuwafikia wadau wa utalii na kuongeza thamani ya mazao yao. Tukiongeza elimu, tunaweza kuwahudumia wateja wengi zaidi,” amesema mwenyekiti huyo.

Ameongeza kuwa kuna haja ya kueneza elimu ya kilimo ikolojia katika vijiji vyote 57 vya wilaya ya Karatu, ili kuongeza uzalishaji wa mazao salama na yenye tija kwa jamii.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Endabashi, Fabian Mussa, amesema atahakikisha anashawishi viongozi wa ngazi za juu ili kuwepo kwa mazingira rafiki yatakayowezesha kilimo ikolojia kukua na kuwafikia wakulima wengi zaidi.

“Tutaendelea kusukuma ajenda hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanapata msaada unaohitajika na kilimo ikolojia kinakuwa chaguo kuu,” amesema Mussa.

Mafunzo na Mnyororo wa Thamani
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea Kituo cha Wakulima Karatu, kilicho chini ya MVIWAARUSHA, kinachotoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima kuhusu kilimo ikolojia, pamoja na utengenezaji wa mbolea na viwatilifu vya asili.
Jimmy Mongi, afisa masoko wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA) amesema kituo hicho kina jukumu kubwa la kuunganisha mnyororo wa thamani wa kilimo ikolojia na kuwasaidia wakulima kupata masoko pamoja na kujiongezea kipato.

“Hapa wakulima wanajifunza kwa vitendo, lakini pia tunauza bidhaa zilizoongezwa thamani na mazao ya wakulima wa kilimo hai ili kusaidia uendelevu wa kituo,” alisema Mongi.

Kilimo ikolojia si tu njia ya kulinda mazingira, bali pia ni fursa ya kiuchumi na kijamii inayowawezesha wakulima kuongeza kipato, kutoa ajira, na kuboresha afya ya jamii. Ushirikiano kati ya wakulima, wajasiriamali, viongozi wa serikali, na taasisi kama IDP, MVIWAARUSHA, RECODA, na SHIWAKUTA, umeonyesha kuwa changamoto zinazokabili kilimo ikolojia zinaweza kushughulikiwa kwa elimu, teknolojia ya asili, na masoko thabiti.

Kwa kuendelea kuwekeza kwenye kilimo ikolojia, wilaya ya Karatu inaweza kuwa mfano wa taifa katika kuendeleza uzalishaji wa chakula salama, afya bora, na maendeleo endelevu kwa wakulima na walaji wote.






Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.