KILIMO IKOLOJIA CHASHIKA KASI ARUSHA, WAFANYABIASHARA 50 WANUFAIKA


ARUSHA.

MFUMO jumuishi uliotengenezwa na Shirika la Islands of Peace (IDP), umewezesha wafanyabishara 50 wa mazao na bidhaa za kilimo ikolojia mkoani Arusha kufuata hatua na taratibu za kibiashara na misingi ya kiikolojia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika wa IDP, Ayesiga Buberwa wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii mwishoni mwa wiki mkoani Dodoma, kuhusu mikakati yao ya kuendeleza kilimo ikolojia nchini.

Ayesiga alisema Mkutano Mkuu wa Wadau wa Kilimo Ikolojia Tanzania (NEOAC), amewasilisha mada inayohusu Maendeleo ya Teknolojia na Mifumo ya Mabadiliko ya Chakula katika Biashara za Kilimo Ikolojia Kaskazini mwa Tanzania.

Pia alibainisha nguvu na changamoto, njia waliojifunzwa na kuendelezwa kwa pamoja kwa ajili ya mpito kuelekea kilimo ikolojia kamili.

Alisema shirika lake limetengeneza mfumo huo ili iweze kusaidia kundi la wafanyabishara ambao wamejikita kwenye kilimo ikolojia.

Ayesiga alisema kufanya biashara ni kitu kimoja na misingi ya biashara ni kitu kingine, hivyo wafanyabishara 50 watatembea nao hadi kufikia muafaka wenye tija kwa pande zote.

"Kubadilika kwenda kwenye kilimo ikolojia ni mchakato na una mambo mengi, kuna vizuizi na fursa, kwa hiyo tunaangalia kwa pamoja tunawezaje kutembea. Tumebuni zana za kutusaidia, tumeweka viashiria ambavyo vitatuonesha sasa tumepiga hatua na kwamba kwenye hili tunaweza kupambania suala lingine," alisema.

Alisema kwa sasa wafanyabiashara 50 wa mkoa wa Arusha na Kilimanjaro wanajihusisha na mazao na bidhaa za kilimo ikolojia.

"Katika mkoa wa Arusha na Kilimanjaro tunajivunia wazalishaji yaani wakulima, wasindikijani, wauzaji sokoni na vyakula kwenye migahawa," alisema.

Ayesiga alisema kundi hilo la wafanyabishara limekuwa likijipima kila baada ya miezi sita, ili kuona kama linafanya vizuri.

Mkurugenzi huyo alisema IDP inapambana kuhakikisha soko la ndani linapata mazao ya kutusha ya kilimo ikolojia kabla ya kukimbia nje.

Mkurugenzi huyo alisema pamoja na jitihada zinazofanywa kusukuma kilimo ikolojia, bado kuna changamoto kama elimu, sera na nyingine ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja kuzitatua.

Kwa upande wake Program Meneja wa Shirika la Biovision, Thomas Kayper alisema Tanzania imefanya vizuri kwenye eneo la kilimo ikolojia, hivyo nguvu inahitajika kuongezwa ili kufikia malengo makubwa.

Alisema kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwitikio wa wakulima kuhamia kwenye kilimo hicho, jambo ambalo linatoa matumaini makubwa kwa wadau. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.