Dar es Salaam.
Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo imetangaza kuwa mwaka huu itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya maombolezo na tafakari, badala ya sherehe, kufuatia vifo na matukio ya ulemavu wa kudumu yaliyoripotiwa wakati wa ghasia za Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo Februari 26, 2026 katika Makao Makuu ya chama hicho Magomeni, Mwenyekiti wa Ngome hiyo, Janeth Rite, alisema bado kuna majonzi makubwa miongoni mwa Watanzania waliopoteza wapendwa wao, huku wengine wakiendelea kuishi na athari za kudumu za matukio hayo.
Alisema mwezi Machi mwaka huu utakuwa maalum kwa maombolezo na shughuli za kuonyesha mshikamano, akisisitiza kuwa ni wakati wa kutafakari, kuombeana na kusimama pamoja kama taifa.
Kwa mujibu wa Rite, Machi 8, 2026 watatumia siku hiyo kufanya maombi na hitma, pamoja na shughuli za kijamii ikiwemo kutembelea wazee na watoto yatima, kufanya usafi katika vituo vya afya, kutoa misaada, kuchangia damu na kuzuru makaburi ya wapendwa wao. Pia mikutano ya hadhara itafanyika katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendeleza wito wa haki na uwajibikaji.
Ngome ya Wanawake itaendelea kuwa sauti ya waliodhulumiwa na kusimamia misingi ya haki, akiahidi kuwa hawatasita kuikumbusha jamii na mamlaka umuhimu wa kutenda haki kwa wote.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Machozi ya Mama ni Deni la Taifa.”

Hakuna maoni: