PPPC YATOA MAFUNZO MAALUM KUSAKA TRILIONI 170 KUTOKA SEKTA BINAFSI

CRDB, TADB NA TPA WAJIPANGA KUNASA FURSA ZA UBIA

Katika kuhakikisha Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano unafanikiwa, Serikali kupitia Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP- Centre) imeanza mkakati wa makusudi wa kutoa mafunzo kwa taasisi za kifedha na makampuni binafsi nchini ili kuyavutia kuwekeza kwenye miradi mikubwa kwa utaratibu wa PPP

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka kituo cha Ubia, Bi . Flora Tenga, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kutoa uelewa sekta binafsi pamoja na taasisi za fedha nchini sera , sheria na fursa zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya PPP.

Bi.Tenga alifafanua nafasi ya PPP katika kutekeleza Mpango huo wa 4 wa miaka 5 ( FYDP4) unaotarajia kuanza Julai 2026 hadi 2031, ambapo Serikali inatakiwa kukusanya rasilimali zenye thamani ya Tsh Trillini 477.

"Katika hizo Trillion 477, asilimia 70 ya fedha hizo zinatakiwa zitoke sekta binafsi na katika hiyo asilimia 70, asilimia 51 (sawa na takribani Trilioni 170) zitatoka kwenye kutekeleza miradi kwa utaratibu wa Ubia (PPP). Kuna miradi mingi ipo tayari kwenye orodha ( PPP pipelines) kutoka sekta mbalimbali kama sekta ya umeme, usafirishaji, uchukuzi, na maji ambazo ni sekta za kipaumbele katika mpango huo" alifafanua Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka kituo cha ubia Bi. Flora Tenga.

Halikadhalika, wadau walioshiriki mafunzo hayo wameeleza utayari wao. Andrew Mbunda kutoka Benki ya CRDB, alieleza kuwa lengo lao ni kujua miradi iliyopo mapema ili benki hiyo iweze kuwezesha fedha kwa wakati na kuepuka ucheleweshaji.

Kwa upande wake, Angelina Nyansambo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) alisema mafunzo hayo yamewapa mwanga wa jinsi ya kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi mikubwa ya kilimo.

Naye Shabani Kiduta, Afisa Mipango kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari TPA, alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kwa sasa, kwani uelekeo wa TPA ni kuwa wamiliki wa miundombinu na kuiachia sekta binafsi kuendesha shughuli za kibandari.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.