SEKTA YA MADINI YACHANGIA 12.7% KIPINDI CHA JULAI HADI SEPTEMBA 2025


Dodoma

Sekta ya madini nchini imeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa uchumi nchini, baada ya kuchangia asilimia 12.7 ya Pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025.

Hayo yameelezwa leo Machi 24, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, wakati akifungua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026, lililofanyika katika ukumbi wa Midland Hotel, jijini Dodoma.


Mauzo ya Madini Yavuka Trilioni 10

Katika hatua nyingine, Eng. Samamba amesema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya madini nje ya nchi kwa mwaka 2025 imefikia dola za Marekani milioni 4,119 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 10.3 za kitanzania.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini, hususan kupitia uanzishwaji na uboreshaji wa masoko ya madini pamoja na mikakati madhubuti ya kudhibiti utoroshaji wa madini.


Wadau Wapongeza Utendaji wa Wizara

Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Afisa Kazi Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmary, amesema Ofisi ya Kamishna wa Kazi inajivunia ushirikiano na mafanikio ya Wizara ya Madini katika kuzingatia masuala ya haki na ustawi wa wafanyakazi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa TUGHE Taifa, Happiness Kitarima, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza kwa vitendo misingi na kanuni za chama hicho, ikiwemo kulinda maslahi ya watumishi na kuimarisha mahusiano kazini.


Mwelekeo wa Sekta Unaendelea Kuimarika

Kwa ujumla, takwimu hizo zinaashiria kuimarika kwa mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa, sambamba na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni na kudhibiti mianya ya upotevu wa rasilimali. Sekta ya Madini inaendelea kuwa miongoni mwa mihimili muhimu katika ajenda ya maendeleo ya uchumi wa viwanda na uwekezaji nchini.  

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.