TAKUKURU TEMEKE YAFUATILIA MATUMIZI YA BILIONI 36.5 KATIKA MIRADI YA MAENDELEO


Temeke, Dar es Salaam.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefuatilia matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 36.5 zilizotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na ujenzi ndani ya halmashauri za manispaa katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2025. 

Akitoa taarifa hiyo kwa umma Naibu Mkuu wa TAKUKURU Temeke Ismail Bukuku, amesema taasisi hiyo imefanya ufuatiliaji huo wakilenga kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi. 

Amesema katika kipindi hicho TAKUKURU ilifuatilia miradi minne ya maendeleo, ambapo pia ilitoa ushauri wa kitaalamu baada ya kubaini dosari katika miradi miwili. Ushauri huo ulitekelezwa na wahusika kwa wakati na kusaidia kurekebisha mapungufu pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hizo zimeongeza uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo la Temeke. 

Aidha, katika eneo la elimu kwa umma, TAKUKURU Temeke imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, haki na wajibu wao katika kuzuia vitendo hivyo pamoja na taratibu sahihi za kutoa taarifa. 

Taasisi hiyo imesema juhudi hizo zimeimarisha ushirikiano kati ya wananchi na TAKUKURU katika utoaji wa taarifa za vitendo vya rushwa, hali iliyochangia kuongezeka kwa taarifa za rushwa kwa asilimia 50 ikilinganishwa na robo iliyopita. 

TAKUKURU imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili kuimarisha uwajibikaji na kulinda rasilimali za umma. 



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.