Dar es Salaam
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema kuwa katika kipindi cha Januari na Februari 2026, jumla ya tani 9.93 za dawa za kulevya aina mbalimbali zimekamatwa katika operesheni zilizoendeshwa nchi nzima.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 4, 2026, Lyimo alisema mbali na dawa hizo, chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa pamoja na kuteketezwa kwa mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 87.5. Aidha, magari sita na pikipiki 29 vilikamatwa huku watuhumiwa 151 wakishikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara hiyo haramu.
Kwa kushirikiana na maafisa wa forodha katika kituo cha Mutukula, Mamlaka ilikamata boksi 105 za Pethidine (chupa 1,045), boksi 31 za Morphine Sulphate (chupa 310) na boksi 44 za Fentanyl (chupa 440). Dawa hizo zilikutwa ndani ya basi la abiria la kampuni ya SR Classic lenye usajili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lililokuwa likisafiri kati ya Uganda, Tanzania na DRC.
Dawa hizo ambazo ni za kundi la afyuni (opioids) hutumika hospitalini kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, wanaougua saratani, ajali au selimundu. Hata hivyo, zikichepushwa kutoka matumizi halali zinaweza kusababisha uraibu na madhara makubwa kiafya ikiwemo kuathiri mfumo wa fahamu, upumuaji na mapigo ya moyo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, dawa hizo zimedhibitiwa kisheria na usambazaji wake unaruhusiwa kufanywa na Bohari ya Dawa (MSD) pekee.
Katika operesheni nyingine jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa mmoja alikamatwa akiwa na kilo 81.883 za bangi aina ya skanka ndani ya gari la mizigo lililokuwa limebeba matunda. Eneo la Chanika Buyuni, watuhumiwa wawili walinaswa na kilo 488.64 za skanka, huku jijini Mbeya watuhumiwa sita wakikamatwa kwa nyakati tofauti wakisafirisha bangi hiyo.
Mkoani Arusha, watu wawili walikamatwa wakiwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilo 363.45, huku operesheni zilizofanyika katika mikoa mbalimbali zikikamata tani 5.24 za bangi, tani 4.04 za mirungi na gramu 72 za heroin.
DCEA imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za Serikali pamoja na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha dawa za kulevya zinadhibitiwa na dawa tiba zenye asili ya kulevya zinawafikia wagonjwa wanaostahili pekee.
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Mamlaka imeeleza, ni jukumu la kila mwananchi.

Hakuna maoni: