Dar es Salaam.
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara zaidi ya Kilomita 56 kwa kiwango cha lami na zege kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mkoani humo.
Akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Ilala, Mhandisi Grayson Nzunda amesema kuwa miradi inayojengwa ni barabara za lami na zege, mifereji ya maji ya mvua, makalavati, njia za waenda kwa miguu, uwekaji wa taa za barabarani pamoja na kuweka alama za barabarani ambapo mradi unagharimu shilingi Bilioni 138.
“Hapa tulipo ni maeneo ya Kivule tupo kukagua ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilomita 12, barabara ya Kivule-Majohe Junction Km 2.79 inajengwa kwa kiwango cha zege na barabara ya Kitunda-Kivule-Msongola Km 9.95 inajengwa kwa kiwango cha lami, mradi umegharimu shilingi Bilioni 30 kati ya Bilioni 138 za wilaya nzima ya Ilala", alisema.
Ameeleza kuwa barabara hizo zilikuwa na changamoto kubwa hivyo kukamilika kwake zitasaidia wananchi kufikia huduma mbalimbali kwa urahisi na kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji, pia barabara hizo zinatumika kama 'bypass' kwa wanaokwenda Chanika au Majohe kama barabara kubwa ikiwa na foleni.
Naye, Bi. Vicky Shayo mkazi wa Kitunda amesema kuwa wamekuwa wakikosa wateja katika biashara zao kutokana na changamoto ya barabara hasa kipindi cha mvua kutokana na maji mengi na matope ambapo inapelekea watu kuanguka kwasababu ya udongo kuteleza, lakini barabara ikikamilika itawasaidia kufanya biashara zao na kipato kitaongezeka.
Bi. Maria Petro mkazi wa Kivule ameishukuru serikali kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwani walikuwa wanapata changamoto kwenda hospitalini lakini sasa hivi usafiri umekuwa rahisi kufika mpaka Banana.
Aidha, Mwenyekiti wa mtaa wa Karume Bw. Hajibu China amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani anaiona Ilala inakwenda kubadilika kutokana na maboresho ya barabara kwani wananchi wanajenga nyumba zao, pia kutakuwa na taa za barabarani zitakazopendezesha mji na kuongeza ulinzi na usalama.








Hakuna maoni: