Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji (EWURA) kuendesha operesheni ya kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya kuficha mafuta kwa makusudi ili kusababisha uhaba katika maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanatumia mwanya wa hali iliyopo kwa kuchukua mafuta kutoka kwenye maghala (depots) kwa kiwango kikubwa kuliko mahitaji yao, kisha kuyahifadhi wakisubiri bei mpya zitangazwe ndipo wayauze kwa bei ya juu.
Amesisitiza kuwa vitendo hivyo ni kosa la uhujumu uchumi, na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria. Hivyo, amewaonya wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwa kuwa vinachangia kuleta uhaba wa mafuta.
“Nimewaelekeza Ewura kuanzia leo, usimwonee mtu yoyote aibu kama mtu akikamatwa ameficha mafuta, kwakweli sisi hatutamvumilia na Kamshna msimamie hilo mafuta yanayopakiwa hapa Dar es salaam muhakikishe yanafika kwenye vituo kama inavyokuwa imepangwa” amesisitiza Matarajio.
Dkt. Mataragio amefafanua kuwa tayari wameanza kupokea taarifa za baadhi ya vituo kukosa mafuta, hali inayochangiwa na vitendo vya aina hiyo ambapo mafuta yanapochukuliwa Dar es Salaam hayafiki katika vituo kama inavyotakiwa.




Hakuna maoni: