WAFANYAKAZI WANAWAKE NDC WATOA MSAADA KWA WANAWAKE WALIOPO GEREZA LA SEGEREA


Dar es Salaam

Wafanyakazi wanawake NDC watoa Msaada kwa Wanawake Waliopo Gereza la Segerea Dar es Salaam Wanawake kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) leo wametembelea Gereza la Wanawake Segerea lililopo wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, na kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa mahabusu wanawake waliopo gerezani hapo. 

Msaada huo umejumuisha sabuni, taulo za kike, sukari pamoja na mifagio, ukiwa ni sehemu ya mchango wa shirika hilo katika kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufikia kilele tarehe 8 Machi 2026.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa niaba ya Shirika la Taifa la Maendeleo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya TUICO Tawi la NDC, Bi. Paula Kasange, alisema ziara hiyo imelenga kuonesha mshikamano na kuwafariji wanawake waliopo gerezani. “Tunashukuru sana uongozi wa Gereza la Segerea kwa kutupokea na kutupa nafasi ya kuweza kuwatembelea akina mama waliopo hapa. Kupitia msaada huu tunataka kuonesha kuwa bado ni sehemu ya jamii yetu na tunawajali,” alisema Kasange.

Aidha, Kasange aliishukuru menejimenti ya NDC pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika hilo kwa kuunga mkono na kuwezesha wanawake wa NDC kushiriki katika zoezi hilo la kijamii.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa menejimenti ya NDC kwa kutuunga mkono katika jitihada hizi, kwani shughuli hii inaendana na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani na pia dhamira ya shirika letu ya kurudisha kwa jamii,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUICO NDC, Bi. Pulkeria Shao, alisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza na kuona juhudi zinazofanywa na mahabusu wanawake katika kujishughulisha na kazi za mikono. “Tumefarijika kuona baadhi ya wanawake waliopo hapa wakijishughulisha na kazi mbalimbali za mikono ikiwemo utengenezaji wa mabegi. Hii inaonesha kuwa hata wakiwa hapa bado wanaendelea kujifunza na kujijengea ujuzi utakaowasaidia baada ya kutoka,” alisema Shao.

Naye Mkuu wa Gereza la Wanawake Segerea, SSP Hamida Matimba, aliushukuru uongozi na wafanyakazi wa NDC kwa kuwatembelea na kutoa msaada huo, akisema hatua hiyo imeleta faraja kubwa kwa wanawake waliopo gerezani.

“Tunawashukuru sana NDC kwa kututembelea na kuleta msaada huu. Msaada kama huu unaonesha upendo na mshikamano kwa wale waliopo katika mazingira haya,” alisema SSP Matimba.

SSP Matimba pia aliiasa jamii, hususan wazazi na akina mama, kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kuepuka tabia hatarishi zinazoweza kuwapelekea kukiuka sheria na hatimaye kujikuta wakiingia kwenye mfumo wa magereza. Zoezi hilo la kutoa msaada ni sehemu ya utamaduni wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) wa kushiriki katika shughuli za kijamii kwa kuangalia makundi maalum katika jamii, ikiwemo mahabusu, wafungwa na makundi mengine yenye uhitaji, ikiwa ni njia ya kuimarisha mshikamano na kuwajali wanajamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.