Na Mwandishi Wetu,
Mafinga.
Wanawake wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiwemo kutoka Shamba la Miti Sao Hill na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wamejitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji Mafinga mkoani Iringa leo Machi 8, 2026, wakitumia jukwaa hilo kuonesha mchango wao katika uhifadhi wa misitu na maendeleo ya taifa.
Katika maadhimisho hayo yaliyowakutanisha wanawake kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliwataka wanawake kuendelea kudumisha umoja na mshikamano ili kuongeza nguvu ya pamoja katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema wanawake wanapaswa kutumia fursa zilizopo kujiongezea uwezo wa kiuchumi na kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao ya kazi ili kuwa mfano bora kwa jamii.
Kwa upande wao, wanawake wahifadhi kutoka Shamba la Miti Sao Hill walisema ushiriki wao katika maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuonesha nafasi kubwa ya wanawake katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Walieleza kuwa kupitia TFS, wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uhifadhi ikiwemo upandaji miti, ulinzi wa misitu na utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya misitu.
Katika maadhimisho hayo pia, wanawake hao walitumia mabanda ya maonesho kutangaza bidhaa zitokanazo na mazao ya nyuki kama vile asali na nta ya nyuki, huku wananchi waliotembelea mabanda hayo wakipata fursa ya kujifunza kuhusu thamani ya mazao hayo katika kukuza uchumi na kuhifadhi mazingira.
Sambamba na maonesho hayo, wanawake wahifadhi walitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda misitu, wakisisitiza kuwa misitu ina mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya nyuki na ustawi wa viumbe hai.
Ushiriki wa wanawake wahifadhi wa TFS katika maadhimisho hayo umeendelea kudhihirisha kuwa wanawake wana nafasi muhimu katika sekta ya uhifadhi wa misitu na wana mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo endelevu ya nchi.








Hakuna maoni: