Mwanza.
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, askari na maafisa wa uhifadhi wa kike kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Kanda ya Ziwa wameendesha zoezi la upandaji miti na utoaji elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii.
Wanawake hao kutoka Hifadhi ya Shamba la Miti Buhindi walipanda jumla ya miti 1,500 katika shule mbili za Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kushirikisha jamii katika uhifadhi wa misitu.
Katika zoezi hilo lililofanyika Machi 6, miti 750 ilipandwa katika Shule ya Sekondari Iligamba iliyopo Kata ya Iligamba, huku miti mingine 750 ikipandwa katika Shule ya Msingi Lushamba iliyopo Kata ya Bulyaheke.
Mbali na kupanda miti, maafisa hao walitoa elimu kwa wanafunzi, walimu na viongozi wa vijiji kuhusu umuhimu wa kupanda na kutunza miti ili kulinda mazingira na rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Zoezi hilo lilishirikisha walimu, wanafunzi pamoja na viongozi wa vijiji husika, likiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wa upandaji miti katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za wanawake wa TFS kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo vinavyochangia maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira.



Hakuna maoni: