ZERA YAZINDUA MAGARI YA UMEME: FURSA MPYA ZA UCHUMI NA NISHATI SAFI NCHINI TANZANIA



Dar es Salaam, Machi 6, 2026.

Serikali na wadau wa sekta ya nishati na usafiri Zera wamefanya uzinduzi rasmi wa magari ya umeme nchini ikiwa ni hatua muhimu itakayofungua ukurasa mpya wa matumizi ya nishati safi, kupunguza gharama za usafiri, kukuza uchumi wa taifa, na kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 06,2026 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, ukiandaliwa na kampuni ya ZERA, inayolenga kutoa suluhisho la usafiri wa kisasa na endelevu nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema mageuzi ya usafiri wa magari ya umeme ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuongeza matumizi yenye tija ya umeme na kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.

“Magari ya umeme si mtindo wa muda mfupi, bali ni mwelekeo wa kimkakati unaosaidia kupunguza gharama za usafiri, kuimarisha mazingira, na kufungua fursa za ajira kupitia viwanda na teknolojia mpya,” alisema Mramba.

Tafiti za United Nations Environment Programme (UNEP) zinaonyesha kuwa usafiri wa umeme unapunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, pikipiki ya petroli inagharimu takribani Sh31,000 kwa siku, huku pikipiki ya umeme ikigharimu Sh3,000 pekee.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZERA, Emmanuel Kazimoto, amesema kampuni yake inalenga kujenga mfumo kamili wa usafiri wa umeme unaojumuisha: uzalishaji wa magari, ufungaji wa miundombinu ya kuchaji, ushauri wa kubadilisha magari ya kampuni kuwa ya umeme, na huduma za matengenezo.

Kazimoto amesema mpango huo utaanza kwa kuingiza magari yaliyo Complete Built-Up (CBU), hatua ya pili itahusisha magari yaliyo Semi Knocked Down (SDU) ili kuongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani, na hatua ya tatu kuanzisha mkusanyiko wa magari hayo hapa nchini.

Katika hatua za mwanzo, ZERA imeingiza baadhi ya magari ya umeme kwa ajili ya maonyesho na majaribio, ikiwa ni pamoja na magari ya abiria na mabasi madogo yanayoweza kutumika katika usafiri wa mijini.

Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha usafiri wa umeme unakuwa endelevu, wa kuaminika, na unaochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.