Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Serikali imesema ukuaji wa biashara mtandaoni unaendelea kuibua changamoto mpya kwa walaji, hali inayohitaji umakini zaidi katika kulinda haki zao na kuhakikisha wanapata huduma na bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema pamoja na fursa zinazotokana na teknolojia, bado kuna mianya ya udanganyifu inayoweza kuwaathiri watumiaji wa huduma hizo.
Alisema serikali imejipanga kuimarisha mifumo ya usimamizi pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi wanapotumia majukwaa ya kidijitali kununua bidhaa au kupata huduma.
Kapinga alionya kuwa wafanyabiashara wanaotumia majukwaa ya mtandaoni kukiuka sheria na taratibu hawatavumiliwa, na kwamba hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa ili kulinda maslahi ya walaji.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa uwazi na uaminifu kwa watoa huduma, akibainisha kuwa mazingira ya kidijitali yanahitaji nidhamu na uwajibikaji wa hali ya juu ili kujenga imani kwa watumiaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC), Agrey Mulimuka, alisema ni muhimu kwa watumiaji kuwa na taarifa sahihi kabla ya kufanya manunuzi mtandaoni ili kuepuka hasara zinazoweza kujitokeza.
Aliongeza kuwa FCC itaendelea kusimamia masoko na kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uwezo walaji kutambua haki zao na kuchukua hatua wanapodhulumiwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa walaji wengi ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki zao katika mazingira ya kidijitali.
Alisema kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji, FCC inalenga kuwasaidia wananchi kutambua bidhaa salama, huduma bora na kujiepusha na udanganyifu unaoweza kujitokeza katika biashara za mtandaoni.
Ngasongwa alisisitiza kuwa mlaji mwenye uelewa ana nafasi kubwa ya kujilinda, huku akiwahimiza wananchi kuwa makini na kutoa taarifa pale wanapokutana na changamoto ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.





Hakuna maoni: