Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 1,983.31 za dawa za kulevya katika operesheni maalum zilizofanyika mwezi Machi, 2026.
Akizungumza leo, Kamishna wa DCEA, Aretas Lymo amesema kuwa pamoja na dawa hizo, pia zilikamatwa kilo 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 pamoja na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Aidha, operesheni hizo zilisababisha kuteketezwa kwa ekari 55.5 za mashamba ya bangi huku jumla ya watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na makosa hayo.
Kwa mujibu wa Kamishna Lymo, takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la ukamataji wa dawa aina ya mirungi, ambapo kilo 1,267.12 zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo.
Alisema hali hiyo inatokana na mkakati wa mamlaka hiyo kujikita zaidi katika operesheni za mashambani, baada ya kufanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.
Katika matukio mbalimbali, jijini Dar es Salaam, eneo la Tegeta Kibo, kilo 101.2 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya basi la abiria aina ya Yutong, lililokuwa likisafiri kutoka Mombasa kuelekea Dar es Salaam. Dawa hizo zilifichwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye mfumo wa hewa (AC) ili kukwepa ukaguzi.
Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni pamoja na dereva Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na abiria wengine watatu.
Katika Mkoa wa Pwani, kilo 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa njiani kuingia Dar es Salaam, huku mkoani Mwanza kilo 52 zilikamatwa katika kizuizi cha Magu na Bandari ya Mwanza South.
Vilevile, wilayani Misungwi, kilo 184.9 za mirungi zilikamatwa ndani ya nyumba na kwenye vyombo vya usafiri, huku watuhumiwa wawili wakihusishwa na tukio hilo.
Mkoani Tanga, kilo 32.95 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya mfuko pamoja na maembe, wakati operesheni nyingine zilinasa kilo 164.01 katika matukio tofauti.
Kwa upande wa Arusha, wilayani Longido, kilo 106.25 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish, ambapo Diwani wa Kata ya Kimokouwa ni miongoni mwa waliokamatwa.
Katika mikoa ya Kilimanjaro, Songwe na maeneo mengine, ukamataji uliendelea ambapo jumla ya kilo 707.995 za bangi zilinaswa.
Kamishna Lymo alibainisha pia kuwa jijini Dar es Salaam, katika hosteli ya wanafunzi iliyopo Kijitonyama, paketi 141 za bangi aina ya skanka zilikamatwa, jambo linaloashiria uwepo wa biashara ya dawa za kulevya karibu na taasisi za elimu.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa jamii, hususan wamiliki wa makazi ya wanafunzi, kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha mazingira ya wanafunzi yanakuwa salama.
Katika hatua nyingine, DCEA ilifanya ukaguzi katika kampuni zinazohusika na kemikali bashirifu pamoja na maduka ya dawa, ambapo kiasi kikubwa cha kemikali kilizuiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria.
Kamishna huyo alisisitiza kuwa kemikali hizo zinaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya endapo hazitadhibitiwa ipasavyo, huku akibainisha kuwa baadhi ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na alprazolam, tramadol na fentanyl, ambazo zinaweza kusababisha uraibu endapo zitatumika vibaya.
Amesema operesheni hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kupambana na dawa za kulevya, huku akionya kuwa bado kuna mitandao mipya inayojitokeza na kubadilisha mbinu za usafirishaji.

Hakuna maoni: