DKT. KIJAJI: MUSTAKABALI WA UCHUMI AFRIKA MASHARIKI UNATEGEMEA UHIFADHI WA RASILIMALI ASILIA

Na John I. Bera, 

Arusha.

Uchumi wa nchi za Afrika Mashariki unategemea namna ukanda huo utakavyolinda, kusimamia na kutumia utajiri wake wa rasilimali asilia.

Akifungua Mkutano wa 11 wa Baraza la Sekta ya Mawaziri wa Mazingira na Usimamizi wa Maliasili (SCENR) la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha tarehe 23 Aprili 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)amesema rasilimali asilia si tu urithi wa kizazi cha sasa, bali pia ni msingi mkuu wa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu kwa nchi wanachama.

Ameongeza kuwa ukanda wa Afrika Mashariki umejaliwa hazina kubwa ya rasilimali asilia, ikiwemo misitu, wanyamapori, vyanzo vya maji safi pamoja na mifumo ya ikolojia ya bahari, ambavyo vinachochea sekta muhimu kama utalii, kilimo, uvuvi na nishati.

Hata hivyo, ameonya kuwa licha ya umuhimu wake katika kukuza uchumi, rasilimali hizo zinakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuwai, uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu. 

Amesema hali hiyo inaathiri moja kwa moja tija ya rasilimali hizo na kuhatarisha sekta muhimu za uchumi pamoja na ustawi wa jamii.

Aidha, Dkt. Kijaji amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa sera za kimkakati za mabadiliko ya tabianchi na kutumia fursa mpya kama masoko ya kaboni pamoja na kutumia mbinu za asili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji ametoa mwaliko kwa nchi wanachama kushiriki katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, akieleza kuwa utakuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ulinzi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani.

Aidha ameongeza kuwa matarajio yake kuwa mkutano huo utazaa matokeo yatakayosaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali asilia na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Zanzibar, Mhe. Hamis Hassan; Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagirwa; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew; pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw. Nkoba Mabula ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.