DSE YATAJWA KUWA FURSA MPYA KWA MASHIRIKA ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imezitaka taasisi na mashirika ya umma kubadilika na kuanza kuchangamkia fursa zinazotolewa na Dar es Salaam Stock Exchange (DSE), hususan katika kuongeza mitaji na kuimarisha uendeshaji wa miradi.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu kati ya DSE na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar. Makubaliano hayo yanalenga kujengeana uwezo na kuongeza ushiriki wa taasisi za umma katika soko la mitaji.

Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Sanya, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha ufanisi wa mashirika ya umma, akibainisha kuwa mchakato wa makubaliano hayo ulianza tangu Machi mwaka huu.

Alisema ofisi yake ina majukumu makubwa ya kusimamia uwekezaji wa serikali, hivyo ushirikiano na DSE utasaidia mashirika kupata njia mbadala za kupata mitaji badala ya kutegemea mikopo ya benki pekee.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Biashara wa DSE, Emmanuel Nyalali, alisema makubaliano hayo yataongeza ushiriki wa taasisi na wananchi kutoka Zanzibar katika soko hilo.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inavyoendelea kuimarisha uchumi wake, tunaamini ushirikiano huu ni hatua muhimu kwa mashirika kujiorodhesha katika DSE,” alisema Nyalali.

Sanya alisisitiza umuhimu wa elimu kuhusu soko la mitaji, akieleza kuwa bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa taasisi nyingi za umma kuhusu fursa zilizopo DSE.

“Hatuwezi kujifungia Zanzibar. Taasisi nyingi zinategemea mikopo ya benki kugharamia miradi. Itafikia hatua benki zitakuwa na ukomo, wakati kuna fursa kubwa katika DSE,” alisema.

Aliongeza kuwa kati ya mashirika 17 ya umma Zanzibar, ni mawili pekee yaliyosajiliwa katika DSE, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza juhudi za uhamasishaji na elimu.

Naye Mkuu wa Idara ya Mitaji Zanzibar, Mustafa Omary Abdallah, alisema makubaliano hayo yataongeza uelewa wa taasisi za umma kuhusu masuala ya uwekezaji na mitaji.

Alieleza kuwa hatua hiyo pia itasaidia serikali kufuatilia kwa karibu uwekezaji wake, ikizingatiwa kuwa imewekeza fedha nyingi katika mashirika hayo na inahitaji kuona tija inayotokana na uwekezaji huo.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa mara moja, huku pande zote zikisisitiza kuwa hayatabaki kwenye makaratasi bali yatazaa matokeo chanya kwa uchumi wa Zanzibar.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.