JUMLA YA WANANCHI 25 WA MBEZI JOGOO WAKOPESHWA MAJIKO SANIFU YA UMEME



DAR ES SALAAM. 

Diwani wa Kata ya Mbezi Juu, Bi. Anna Lukindo, ameipongeza TANESCO chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Lazaro Twange, kwa jitihada za kutekeleza ajenda ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Pongezi hizo zimekuja kufuatia utekelezaji wa mpango wa pili wa ugawaji wa majiko ya umeme kwa mkopo nafuu kwa wakazi wa Mbezi Jogoo, ambapo jumla ya wananchi 25 tayari wamenufaika na mpango huo.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Bi. Lukindo amesema mpango huo ni ushahidi wa dhamira ya TANESCO katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia nishati salama na rafiki kwa mazingira.

“Naipongeza sana TANESCO kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Zoezi hili linaakisi dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza ufanisi wa matumizi ya umeme, na kuendeleza ajenda ya maendeleo endelevu,” alisema.

Aidha, Diwani huyo amewataka wakazi wengine wa kata hiyo kuchangamkia fursa hiyo ya kupata majiko ya umeme kwa mkopo nafuu.

 Amebainisha kuwa walengwa watalipa kwa utaratibu rahisi kupitia manunuzi ya umeme (LUKU) ndani ya kipindi cha miezi 12.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja, Bi. Winifrida Peter, ametoa elimu kwa wananchi mara baada ya kukabidhiwa majiko hayo, akisisitiza matumizi sahihi na salama ya vifaa hivyo ili kulinda afya zao pamoja na mazingira.

Mpango huo unaendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa jamii, ukihamasisha matumizi ya nishati safi kama sehemu ya safari ya kuelekea maendeleo endelevu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.