Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Shirika la Posta Tanzania limeingia makubaliano ya ushirikiano na waendesha bodaboda na bajaji kupitia Chama cha Bodaboda na bajaji wilaya ya kinondoni (CHABBOWIKI) kwa ajili ya kuimarisha huduma ya usafirishaji wa vifurushi na abiria kwa njia ya kidijitali kupitia mfumo mpya wa SwifPack. Makubaliano hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini wa nyaraka za ushirikiano, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta, Ferdinand Kabyemela, alisema SwifPack inalenga kurahisisha usafirishaji wa vifurushi na abiria kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.
Alisema huduma hiyo tayari imepangwa kuanza kutumika nchi nzima, ikianza katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kabla ya kusambazwa maeneo mengine ya nchi ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi. “Dhamira yetu ni kuona SwifPack inakuwa suluhisho la kitaifa katika sekta ya usafirishaji kwa kutumia teknolojia,” alisema.
Kabyemela aliongeza kuwa katika hatua za awali, madereva wa bodaboda na bajaji watapata fursa ya kujiunga na mfumo huo bila makato ya kamisheni, ikiwa ni motisha ya kuwavutia wengi kuingia kwenye huduma hiyo. Pia alibainisha kuwa Shirika la Posta linaendelea kuboresha mfumo wake ili uweze kufanya kazi hata katika mazingira yenye changamoto za upatikanaji wa intaneti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHABBOWIKI, Renfred Madiko, alisema makubaliano hayo ni fursa muhimu kwa waendesha bodaboda na bajaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbana na changamoto katika mifumo mingine ya kidijitali ya usafirishaji.
Alieleza kuwa baadhi ya mifumo hiyo imekuwa ikitoza makato hadi asilimia 28 ya mapato ya madereva, huku SwifPack ikianza kwa ofa ya kutotoza kamisheni kabisa katika kipindi cha awali.
Madiko aliwataka waendesha bodaboda na bajaji nchini kuchangamkia fursa hiyo ili kuongeza kipato na kuboresha huduma za usafirishaji.



Hakuna maoni: