TEMBO CARD YA CRDB BANK YAWAPELEKA WANNE MAREKANI, WATATU WAJINYAKULIA TV JANJA INCHI 85 🔥

Na Mwandishi Wetu,

Benki ya CRDB Bank imeanza rasmi kuwazawadia wateja wake kupitia kampeni ya “Mpango na Tembo Card Visa”, ambapo washindi wa kwanza wamepatikana katika droo iliyochezeshwa leo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza matumizi ya kadi katika kufanya malipo mbalimbali.


Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya benki hiyo, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi, Karington Chahe, amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya kadi badala ya fedha taslimu, sambamba na kutoa zawadi nono kwa wateja watakaoshiriki.

Amesema katika droo ya kwanza, jumla ya washindi saba wamepatikana, ambapo wanne wamejishindia safari ya kwenda Marekani kushuhudia fainali za FIFA World Cup 2026, huku wengine watatu wakijishindia runinga janja (Smart TV) za inchi 85 zenye king’amuzi kilicholipiwa.

“Katika awamu hii ya kwanza tumepata washindi saba, wanne watasafiri kwenda Marekani kuangalia Kombe la Dunia, na watatu wamejishindia TV kubwa za kisasa zenye vifurushi tayari,” amesema Chahe.

Washindi wa safari ya kuelekea Marekani ni pamoja na Kenneth Masana Bina (Kagera), Gasper Melkiory Kavishe (Morogoro), Arnold John Samugabo (Dar es Salaam) na Erick Harison Mlinga (Dar es Salaam).

Kwa upande wa zawadi ya runinga, waliojishindia ni Samson Charles Mkumbo (Dar es Salaam), Theresia Kennedy Mawalla (Dar es Salaam) pamoja na Eunice Aloyce Masigati (Dodoma).

Chahe ameongeza kuwa kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Machi 12, 2026, ikiwa na lengo la kuwapa Watanzania fursa ya kipekee ya kusafiri kwenda kushuhudia moja ya mashindano makubwa zaidi ya soka duniani yatakayofanyika kwa pamoja katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Aidha, amebainisha kuwa jumla ya washindi 20 wanatarajiwa kupatikana mwishoni mwa kampeni hiyo itakayokamilika mwezi Juni mwaka huu, ambapo 10 watapata nafasi ya kusafiri kwenda kushuhudia Kombe la Dunia, huku wengine 10 wakijishindia TV janja.

Kampeni hiyo pia inasindikizwa na balozi wake maarufu, DJ Ally B, anayehamasisha matumizi ya kadi kwa njia ya kisasa zaidi.

CRDB Bank imeendelea kusisitiza wateja wake kutumia Tembo Card Visa katika miamala ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kushinda zawadi hizo, huku droo nyingine zikitarajiwa kufanyika katika kipindi chote cha kampeni hadi Juni mwaka huu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.