Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Mabadiliko ya bei za mafuta nchini kwa mwezi Aprili 2026 yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na vita inayoendelea kati ya Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran, iliyoanza Februari 28, 2026.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji na gharama za mafuta katika soko la dunia, hali inayosababisha kupanda kwa bei hapa nchini.
Katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, EWURA imeeleza kuwa mashambulizi yaliyolenga visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta pamoja na viwanda vya kusafisha mafuta (refineries) yameathiri uzalishaji katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Aidha, Iran kufunga Lango la Hormuz—ambalo hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani—kumeongeza changamoto katika usambazaji wa nishati, hasa kwa nchi zinazoagiza mafuta kutoka ukanda huo ikiwemo Tanzania.
EWURA imeongeza kuwa hali hiyo pia imesababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mafuta kutokana na uhaba wa meli za mizigo, sambamba na kuongezeka kwa gharama za bima kwa meli hizo kutokana na hatari ya vita.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika mwezi Aprili 2026, gharama za kuagiza mafuta (premiums) kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 15.3 kwa mafuta ya petroli na dizeli, hali inayotarajiwa kuendelea kuathiri bei za rejareja nchini.

Hakuna maoni: