WANA-CHATO WAHAMASISHWA KUWA MABALOZI WA UHIFADHI


Na Mwandishi Wetu, 

Geita.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (mb), amewataka wananchi wa Wilaya ya Chato na Watanzania kwa ujumla kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira, akisisitiza kuwa kazi inayofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni msingi wa usalama wa taifa na dunia katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza jana Aprili 16, 2026, mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Silayo, mkoani Geita, Waziri Kijaji aliwapongeza wahifadhi na watumishi wa TFS kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uchumi wa kijani.

“Hapa ni kazi na utu. Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma niwaambie kazi yenu ni nzuri. Mnayafanya mazingira haya kuwa salama si tu kwa Tanzania, bali kwa dunia nzima,” alisema Mhe. Dkt. Kijaji.

Alisisitiza kuwa tafsiri ya “mazingira mazuri” siyo lazima iwe mijini, akieleza kuwa maeneo ya misitu na hifadhi ndiyo nguzo ya afya ya binadamu na ustawi wa mazingira, huku akionya kuwa sehemu kubwa ya magonjwa mijini inachangiwa na uharibifu wa mazingira.

Katika ziara hiyo, Waziri alionesha kufurahishwa na juhudi za TFS katika shughuli za uhifadhi, ufugaji nyuki na ushirikishwaji wa jamii, huku akiitaka taasisi hiyo kuimarisha zaidi mikakati ya kupanua upandaji miti na kuendeleza utalii ikolojia.

Aliitaka TFS kuandaa mipango ya kimkakati ya miradi ya utalii yenye tija kwa jamii na kuomba uwezeshaji kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL) ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa, akisisitiza kuwa juhudi hizo zitaifanya TFS kuendelea kufanya kazi kama timu moja yenye maono ya pamoja.

Awali, akiwasilisha taarifa ya shamba hilo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali, Dkt. Zainabu Bungwa, alisema Shamba la Miti Silayo lilianzishwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa lengo la kurejesha maeneo yaliyoharibika kwa kupanda miti ya kibiashara na kulinda vyanzo vya maji.

Alibainisha kuwa kupitia mradi mkubwa unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wenye thamani ya Euro milioni 41.9, TFS inapanga kuongeza kasi ya upandaji miti katika mashamba ya Silayo (Chato), Wino (Iringa) na Mtimbwa (Mvomero), pamoja na kuimarisha uhifadhi wa mikoko katika Wilaya za Kibiti na Kilwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Bungwa, shamba la Silayo linatarajiwa kuongeza upandaji kutoka hekta 800 hadi hekta 3,000 kwa mwaka, huku jumla ya hekta 15,000 zikitarajiwa kupandwa ndani ya miaka 5 ijayo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe kwa niaba ya mbunge mwenzake, alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kueleza kuwa uwekezaji wa TFS umebadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya mazingira katika eneo hilo.

Alikiri kuwa awali kulikuwa na upinzani kutoka kwa wananchi kuhusu upandaji miti, lakini sasa jamii imeanza kuona manufaa yake na kuunga mkono juhudi za uhifadhi.

“Leo hakuna mwananchi atakayepinga juhudi hizi. Mazingira yamebadilika na tunajivunia kazi inayofanywa na TFS, na niombe muongeze nguvu kwenye jimbo langu ili nalo tuwe na shamba lenye hadhi kama hii,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, alisema Shamba la Miti Silayo ni la pili kwa ukubwa nchini baada ya Sao Hill, na lina uwezo mkubwa wa kuchangia uchumi kupitia mazao ya misitu na utalii, akielekeza pia kuwa andiko la utalii wa Silayo ‘Silayo Utalii’ limfikie mapema kwa ajili ya hatua zaidi.

Alieleza kuwa moja ya mafanikio makubwa ya ziara hiyo ni kubadilika kwa mtazamo wa viongozi wa kisiasa, akiwemo mbunge aliyeshiriki ziara hiyo, na sasa kuwa balozi wa uhifadhi.

Kwa ujumla, ziara ya Waziri Kijaji imeacha ujumbe mzito wa kuhimiza ushirikiano kati ya serikali, taasisi na wananchi katika kulinda rasilimali za misitu, huku ikifungua fursa mpya za kiuchumi kupitia utalii na matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.