SERIKALI YAONGEZA NGUVU MAPAMBANO DHIDI YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

 


Na. Beatus Maganja, 

Dodoma

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu ili kulinda maisha ya wananchi, mali zao pamoja na kuimarisha uhifadhi endelevu wa rasilimali za maliasili nchini.

Hayo yameelezwa leo Mei 15, 2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.), wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha doria katika maeneo yanayokumbwa na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kupitia askari wa uhifadhi pamoja na vikosi maalum vinavyotoa huduma za haraka pale matukio yanapotokea.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza athari za migongano hiyo ili kulinda maisha ya wananchi na mali zao sambamba na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa rasilimali zetu za Taifa,” amesema Dkt. Kijaji.

Amesema matumizi ya teknolojia kupitia mfumo wa Problem Animal Information System (PAIS) yameendelea kusaidia kurahisisha usimamizi wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuharakisha utoaji wa kifuta jasho na machozi kwa wananchi walioathirika.

Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kuhusu namna bora ya kujikinga dhidi ya madhara yatokanayo na wanyamapori hao sambamba na kutumia mbinu mbalimbali za kudhibiti wanyamapori kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi ikiwemo matumizi ya uzio wa nyuki, pilipili, fataki maalum pamoja na kuimarisha mipaka ya maeneo ya hifadhi.

Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi pamoja na wananchi katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni msingi muhimu wa mafanikio ya uhifadhi endelevu nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.