DAR ES SALAAM.
Kutoka kwenye jukwaa la muziki hadi kwenye skrini za filamu, msanii maarufu Barnaba Classic ameonyesha kuwa kipaji chake hakina mipaka baada ya kuzindua rasmi tamthilia yake mpya inayokwenda kwa jina la Kikulacho.
Katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo, Barnaba alisema kuwa tamthilia hiyo ni sehemu ya safari yake mpya katika tasnia ya filamu, akibainisha kuwa msimu wa kwanza utaanza kurushwa kupitia majukwaa ya kidijitali, ikiwemo YouTube, ili kuwafikia mashabiki wake ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumzia maudhui ya tamthilia hiyo, Barnaba alisema Kikulacho imejikita katika simulizi za maisha halisi, ikigusa kwa undani masuala ya usaliti ndani ya ndoa, urafiki na mahusiano, mambo ambayo yamekuwa yakigusa jamii kwa kiwango kikubwa.
"Ni hadithi ambayo watu wengi watajiona ndani yake. Ina mafunzo, burudani na ujumbe unaoakisi maisha ya kila siku," alisema Barnaba.
Tamthilia hiyo imetayarishwa chini ya kampuni ya High Table Films, ambayo ipo chini ya usimamizi wa Barnaba mwenyewe, jambo linaloonyesha dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika kazi za ubunifu na kukuza tasnia ya filamu nchini.
Uzinduzi wa Kikulacho unaongeza orodha ya wasanii wa muziki wanaovuka mipaka ya sanaa zao za awali na kuingia kwa mafanikio katika ulimwengu wa filamu, huku mashabiki wengi wakisubiri kwa hamu kuona kile ambacho Barnaba amekiandaa katika tamthilia hiyo mpya.Heading: Barnaba Aingia Rasmi Kwenye Ulingo wa Tamthilia, Azindua ‘Kikulacho’

Hakuna maoni: