Dar es Salaam
Waumini wa Kiislamu kupitia Tanzania Muharram Community wamefanya maandamano ya amani yenye lengo la kuadhimisha kumbukizi ya Imam Hussein (A.S.), mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W.), huku wakitoa wito wa kudumisha amani, umoja na mshikamano katika jamii.
Kumbukizi za Imam Hussein huadhimishwa kila mwaka katika mwezi wa Muharram, ambapo Waislamu wengi hukumbuka maisha yake na tukio la kuuawa kwake katika Karbala mwaka 680 BK. Kwa waumini wengi, tukio hilo ni ishara ya kusimamia haki, uadilifu na kupinga dhuluma licha ya changamoto.
Katika maeneo mbalimbali duniani, maadhimisho hayo hufanyika kwa njia tofauti kulingana na mila na desturi za jamii husika, ikiwemo mikusanyiko ya dua, mihadhara ya kidini na maandamano ya amani yanayobeba ujumbe wa mshikamano, utu na kuishi kwa kuheshimiana.
Akizungumza wakati wa maandamano hayo, Sheikh Mkuu wa TIC Hemed Jalala amesema tukio hilo linafanyika kukumbuka historia ya Imam Hussein na kujifunza maadili ya utu, haki na ubinadamu ambayo yanaendelea kuwa muhimu katika jamii ya sasa.
Alisema maadhimisho hayo pia yanalenga kuwakumbusha waumini na jamii kwa ujumla umuhimu wa kuishi kwa upendo, mshikamano na kuheshimiana bila kujali tofauti zilizopo.
Naye Bi Zainabu alisema lengo la maandamano hayo ni kufikisha ujumbe wa Imam Hussein wa kuhubiri amani, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanadamu.
Aliongeza kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba binadamu ili waishi kwa umoja, ushirikiano na amani, hali ambayo huchangia ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.









Hakuna maoni: