SAMIA AHITIMISHA ZIARA YAKE KWA KUNADI TANZANIA JUKWAA LA BIASHARA ST. PETERSBURG

Na Beda Msimbe, TBN,

St. Petersburg

Rais Samia Suluhu Hassan leo anahitimisha ziara yake nchini Urusi kwa kushiriki Kongamano la Kibiashara la Tanzania na Urusi pamoja na Jukwaa la Kimataifa la Biashara la St. Petersburg.

Katika jukwaa hilo, Rais Samia anatarajiwa kuinadi Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na biashara kwa kueleza fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uchumi.

Ziara ya Rais Samia imeelezwa kuwa na mafanikio makubwa, hususan katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi kwenye maeneo ya elimu, maendeleo ya rasilimali watu, teknolojia na uwekezaji.

Ziara hiyo imefanyika wakati Tanzania ikiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi na kulifanya taifa kufikia pato la dola za Marekani trilioni moja kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2024.

Akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti wa mwaka 2025/2026 na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2026/2027 bungeni Dodoma hivi karibuni, Balozi Omar alisema ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, pamoja na kuimarika kwa shughuli za kilimo.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, shughuli za ujenzi wa umma na binafsi, pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, usafirishaji na huduma za jamii.

Ziara ya Rais Samia nchini Urusi inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili huku Tanzania ikiendelea kutafuta masoko, teknolojia na uwekezaji kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi.



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.