Naibu Katibu Mkuu asema uzoefu wao bado unahitajika, awataka kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi baada ya kustaafu.
Na Mwandishi Wetu,
Dodoma
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuthamini mchango wa watumishi wake kwa kuwaaga rasmi watumishi 85 waliostaafu katika miaka ya fedha 2024/2025 na 2025/2026, huku ukiwataka kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi na maendeleo ya taifa hata baada ya kumaliza utumishi wa umma.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wastaafu hao iliyofanyika Juni 24, 2026 katika Ukumbi wa Mesuma jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, alisema serikali na wizara vinatambua mchango mkubwa walioutoa katika kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu nchini.
Alisema utumishi wao umeacha alama muhimu katika sekta ya misitu na kwamba uzoefu wao bado unahitajika katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.
“Wizara inatambua mchango wenu na taifa linajivunia uzalendo mlioonyesha katika kipindi chote cha utumishi. Kustaafu si mwisho wa jukumu la kuhifadhi mazingira na rasilimali za taifa; tunawaomba muendelee kuwa mabalozi wa uhifadhi katika maeneo mnayoishi,” alisema Mabula.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Luteni Mstaafu Chiku Abdallah Galawa, alisema hafla hiyo haikuwa ya kuagana pekee bali ni fursa ya kutambua na kusherehekea mchango wa watumishi waliolitumikia taifa kwa uadilifu na kujituma.
Alisema wastaafu hao wanapaswa kuwa mfano kwa watumishi waliobaki kazini na kwamba kila mtumishi anapaswa kujifunza umuhimu wa kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu.
“Leo si siku ya kuagana tu, bali ni siku ya kuthamini na kusherehekea mchango wenu. Ni ukumbusho kwamba kila mmoja wetu atafikia hatua ya kustaafu, hivyo ni muhimu kujiandaa mapema,” alisema Galawa.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi wake ili kuwawezesha kuingia katika maisha mapya kwa utayari na ufanisi.
Alisema TFS itaendelea kuthamini mchango wa watumishi wake waliostaafu kwa kuwa wao ni sehemu ya historia ya mafanikio ya taasisi hiyo katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Menejimenti ya TFS Makao Makuu, wakuu wa kanda na vituo vya TFS pamoja na watumishi kutoka Makao Makuu na Kanda ya Kati.








Hakuna maoni: